19 November 2012

CHADEMA wazua jambo Arusha



Na Pamela Mollel, Arusha

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani Arusha, kinakusudia kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo zilitumika kufanya uzinduzi wa jiji hilo hivi karibuni.

Uamuzi huo umefikiwa na madiwani wa chama hicho wilayani humo ambapo akizungumza kwa niaba yao, Diwani wa Kata ya Levolosi, Efatha Nanyaro, alisema fedha zilizotumika katika
uzinduzi huo zilipaswa kupitishwa na Baraza la Madiwani.

Alisema wahusika wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani ni pamoja na Meya wa jiji hilo, Mkurugenzi na Mweka Hazina.

Kaimu Mkurugenzi wa jiji hilo, Bw. Omari Mkombole, alisema uzinduzi huo ulitumia zaidi ya sh. milioni 123 ambapo kati ya fedha hizo, wadau mbalimbali walichangia kwa ajili ya shughuli hiyo na bajeti hiyo ilipitishwa na madiwani wa vyama vyote.

“Vikao vya kupitisha bajeti hii vilihudhuriwa na madiwani wa vyama vyote kikiwemo TLP, CHADEMA na CCM chini ya Meya wa jiji hili, bajeti halisi ilikuwa sh. 123,689,550, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Arusha (AUWSA), walichangia sh. 18,156,500 ambazo zilikarabati mnara wa Azimio la Arusha.

Alisema Kampuni ya Jiangxi Geo Engeneering (Group) Corporation inayojenga barabara za jiji hilo, ilichangia sh. milioni 12, kampuni ya China Railway Seventh Group Co Ltd, sh. milioni nne.

“Halmashauri ya Jiji la Arusha ilitumia sh. 89,533,050 kugharamia mambo mbalimbali katika sherehe hizi, kuwalipa wasanii ambao walialikwa, chakula kwa Rais Jakaya Kikwete, msafara wake na wageni waalikwa katika Hoteli ya Mt. Meru,” alisema.

Aliongeza kuwa, kamati iliyokuwa inasimamia chakula cha Rais Kikwete, ilikuwa ikiongozwa na Bw. Nanyaro akishirikiana na Diwani wa Mashono, Bw. Paul Mathysen (CCM).

Alisema ushiriki wa viongozi hao ambao ni wawakilishi wa wananchi jijini Arusha, ulionesha kuwa suala hilo lilifanyika
kwa ridhaa ya Baraza la Madiwani kwa niaba ya wananchi.

Uzinduzi wa jiji hilo ulifanyika Novemba mosi mwaka huu ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment