19 November 2012

Mfungwa adakwa na silaha za kivita *Alihukumiwa miaka 15 gerezani mwaka 2010 *Haifahamiki alitorokaje, RPC ashikwa butwaa



Na Suleiman Abeid, Shinyanga

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Jeshi la Polisi, mkoani Simiyu linamshikilia mfungwa ambaye bado anatumikia kifungo cha
miaka 15 gerezani, mkazi wa Kijiji cha Ng’wang’wali, Bw.
Masanja Maguzu (42), baada ya kukutwa na silaha za kivita.

Bw. Maguzu alihukumiwa kifungo hicho mwaka 2010, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Shinyanga baada ya
kukutwa na bunduki aina ya SMG, iliyokuwa na risasi 622.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi, alisema Bw. Maguzu alikamatwa juzi
nyumbani kwake Kijiji cha Ng'wang'wali, wilayani Itilima.

Alisema mbali ya kukamatwa na bunduki hiyo, pia alikutwa
na risasi 31 pamoja na magazini tatu ambazo kati ya hizo, moja hutumika katika bunduki aina ya Uzi Gun, iliyotengenezwa nchini Israel.

“Hivi sasa tunafanya uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira yaliyosababisha mfungwa huyu kuwa nje ya gereza baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 15, hivi sasa amekamatwa
tena kwa kosa la kupatikana na silaha kinyume cha sheria.

“Novemba 6 mwaka huu, polisi walimkamata mke wake anayeitwa Holo Mabuga (30), akiwa na silaha nyingine ya kivita aina ya G.3, risasi zake 36, pamoja na risasi nyingine zinazotumika katika bunduki aina ya SMG,” alisema.

Kamanda Msangi aliongeza kuwa, Bw. Maguzi alikamatwa
siku 10 baada ya kukamatwa mkewe hivyo inawezekana kuwa alitoroka gerezani katika mazingira ya kutatanisha lakini bado
aliendelea kujihusisha na vitendo vya ujambazi na ujangili
katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

“Tukio hili limetushtua sana, wakati tukipambana ili kukabiliana na uhalifu na wahalifu, bado kuna watu wanakwamisha juhudi hizi, huyu mfungwa watu wengi wanajua yuko gerezani anatumikia kifungo chake, ajabu leo kukutwa uraiani,” alisema.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi umebaini kuwa, mke wa mfungwa huyo pamoja na kupatikana na silaha hiyo hakuwa peke yake anapokwenda kufanya uhalifu bali nyuma yake kuna kundi la watu ambao amekuwa akishirikiana nao.

Alisema kupatika kwa magazine ya Uzi Gun kunathibitisha kuwa bunduki yake ambayo matumizi yake ni sawa ya SMG, bado iko mikononi mwa mtandao wa wahalifu.

“Kama bunduki hii haitapatikan haraka, itaendelea kusumbua wananchi, kuhatarisha usalama wa maisha na mali zao pamoja
na wanyama waliopo katika hifadhi,” alisema Kamanda Msangi.

No comments:

Post a Comment