04 October 2012

'Wenyeviti wa mitaa wapewe elimu ya PETS'



Na Stella Aron

TAASISI ya Kupambana na Kupunguza Umaskini (MPR) imeshauri Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na kamati mbalimbali za maendeleo, kupatiwa elimu ya Matumizi ya Fedha za Umma (PETS), ili kusaidia upatikanaji wa maendeleo ya haraka.

Mwenyekiti wa MPR, Bw. Godfrey Kafuru, aliyasema hayo Dar es Salaam hivi karibuni katika mkutano uliofadhiliwa na taasisi ya Foundation For Civil Society, kuhusu matumizi ya fedha ambazo zinatolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mkutano huo ulishirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa na wawakilishi wao kutoka Kata za Kibamba na Mbezi ili kuwajengea
uwezo wa mbinu na stadi za ufuatiliaji matumizi ya fedha hizo.

Katika mkutano huo, baadhi ya viongozi wa mitaa walishindwa kutoa majibu kwa wajumbe kuhusu bajeti za maji zinazopangwa kwenye mitaa yao kwa sababu ya kukosa uelewa kuhusu PETS.

“Tumeona ipo haja ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, madiwani na kamati mbalimbali katika kata kupewa elimu inayohusiana na fedha za PETS, wengi wao wameshindwa kutoa majibu kuhusu fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya kutatua tatizo la maji,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa MPR, Bw. Bakari Mngoya, alisema taasisi hiyo imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi ambapo wajumbe wamebaini matatizo mengi yanayokwamisha ukosefu wa maji.

“Yapo matatizo mengi yanayochangia ukosefu wa maji lakini baadhi ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, wamekiri kukosa ushirikiano na madiwani wanapotatua kero za wananchi hasa suala la maji.

“Sisi tutashirikiana nao ili kuhakikisha tatizo kubwa la maji linapungua katika kata zao,” alisema.

Naye mhasibu wa MPR Bw.Issa Mfinanga, alisema kuwa tatizo lililopo ni wenyeviti wa mitaa kutofahamu fedha za ruzuku zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya maji kwenye mitaa yao na kusababisha tatizo hilo kushindwa kufuatiliwa kwa karibuni kwa ushirikiano na wananchi.


No comments:

Post a Comment