04 October 2012
CKHT chatakiwa kushirikiana na serikali
Na Mariam Mziwanda
CHUO Kikuu Huria nchini (CKHT), kimetakiwa kushirikiana na Serikali ili wataalamu wake wa utafiti katika sekta ya kilimo na uchumi waweze kuchochea maendeleo ya nchi.
Bi. Regina Lowassa ambaye ni mke wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Bw. Edward Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika maadhimisho ya miaka 20 ya chuo hicho.
Alisema Kitivo cha Utafiti na Elimu ya Juu ya Uzamili na Uzamivu kina wataalamu ambao wana mchango mkubwa kwa jamii katika kuchochea maendeleo ya nchi.
“Tafiti nyingi zinazotengenezwa na wahitimu wa chuo hiki huwa chachu ya kuibua mambo mbalimbali hivyo ambayo yakitumika vizuri tutapiga hatua ya maendeleo,” alisema Bi. Lowassa.
Alisema hali ya ushirikishwaji watafiti nchini katika maendeleo itasababisha vyuo vingi kuimarisha vitengo vya utafiti kutokana na kuthaminika kwa michango yake.
Mmoja wa wahitimu wa CKHT katika Shahada ya Udhamili Bw. Mudhihiri Mudhihir, alisema anajivunia elimu aliyonayo ambayo ameipata katika chuo hicho.
“Chuo hiki kimetoa fursa ya pekee kwa Watanzania wa hali ya chini kutokana na gharama nafuu ya elimu ya utafiti ambayo wanaitoa kwani itasaidia ongezeko la teknolojia,” alisema na kuongeza kuwa, kama wasomi waliopo katika chuo hiki watatumika ipasavyo kwenye tafiti za maendeleo jamii kubwa itanufaika,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Emmanuel Mbogo ambaye ni Mkuu wa Kitivo cha Utafiti, Udhamili na Uzamivu ngazi ya Stashada na Phd chuoani hapo, amesifu juhudi za Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment