04 October 2012

Mpasuko Jimbo la Mwibara umalizwe


Na Raphael Okello.

KATIBU  mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) ni mzaliwa wa kata ya Iramba, jimbo la Mwibara wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Historia ya jimbo hili kisiasa sio nzuri kutokana na kuwepo kwa kila dalili kwamba ipo mitazamo iliyojikita zaidi katika maslahi ya kiukoo.

Bw. Wilson Mukama anayo nafasi kubwa na heshima inayoweza kumfanya kukaa na viongozi na wanachama wa CCM katika jimbo la Mwibara na kuwaeleza athari za siasa za chuki na kubaguana.

Ni kweli wakati wa kugombea kunakuwepo na makundi ambapo kila mgombea anajaribu kuvutia upande wake kwa ushawishi ili jamii imkubali.

Lakini siasa iliyo nzuri ni kuua makundi baada ya kumpata mshindi hasa kwa wale wanaotoka chama kimoja isitoshe hata wanaotoka vyama tofauti wanapaswa kuacha kubaguana bali watofautiane kwa sare.

Kwa muda mfupi nilioishi wilayani Bunda nikifanyakazi yangu ya uandishi wa habari nimebaini dalili ambazo si nzuri kuhusu mienendo ya kisiasa ndani CCM wilaya ya Bunda hasa jimbo la Mwibara lakini hata kwa vyama vya upinzani.

Hali hii ikiruhusiwa kuendelea ni hakika jimbo la Mwibara itabaki nyuma kimaendeleo si kwamba serikali haitaki kufanya maendeleo huko lakini ni kutokana na  hulka na asili ya wakazi wa jimbo hilo wanaweza kukosa wawakilishi wazuri.

Katika chaguzi zinazoendelea ndani ya CCM wilayani Bunda, jimbo la Mwibara limepoteza uwakilishi katika nyadhifa zote za juu za chama wilayani Bunda.

Ngazi zote za uongozi zimechukuliwa na jimbo la Bunda hivyo kiuwakilishi japo ni wilaya moja lakini kuna pengo kubwa katika utoaji uamuzi kiuwiano.

Wilaya ya Bunda ina kata 28, kata 12 zinaunda jimbo la Mwibara wakati kata 16 zinaunda jimbo la Bunda lakini uwingi wa kata hauwezi kufanywa kigezo cha uwakilishi wote kupelekwa jimbo la Bunda.

Miaka mitano iliyopita mwenyekiti wa CCM wilaya alitoka jimbo la Mwibara lakini ni yeye pekee jina lake lilijitokeza tena ili aweze kutetea kiti japo amebwaga katika uchaguzi huo.

Katika nafasi zingine za NEC, wajumbe wa mkutano mkuu taifa, wajumbe wa mkutano mkuu mkoa, wajumbe halmashuri kuu ya wilaya, uenezi, nafasi ya uchumi na mipango hazikupata mwakilishi kutoka jimbo la Mwibara wakati ni sehemu ya wilaya ya Bunda hii ni ajabu.

Uwakilishi wa Mwibara katika masuala ya  chama sasa imebaki na Mbunge wa jimbo hilo Bw. Alfaxad Kangi na madiwani wa jimbo la Mwibara pekee labda busara itumike baadhi ya wanachama wachaguliwe katika kamati ya siasa ya wilaya.

Lakini pia itategemea utashi na busara wa Mwenyekiti aliyechaguliwa katika kutumia madaraka yake kuhakikisha kuwa Mwibara haiachwi nyuma katika masuala ya maendeleo ya wilaya nzima.

Katika chaguzi hizi ni wazi kwamba wagombea wapo waliotoka jimbo la Mwibara lakini ushawishi mkubwa umetumika kutoka Mwibara ukiwapinga wagombea hao wote wasipate nafasi ya uongozi.

Ushawishi huo haukufanywa na wagombea kutoka jimbo la Bunda lakini unadaiwa kufanywa na baadhi ya wanasiasa wakongwe na watu maarufu wa jimbo la Mwibara.

Lakini lengo la kufanya hivyo ni kwa madai kuwa baadhi ya wagombea hao walikuwa wakiunga mkono ubunge wa Bw. Kangi

Kundi linalodaiwa kutumia mbinu hizo hata kuwashawishi wajumbe kutoka jimbo la Bunda wasiwapigie kura ni lile linalompinga mbunge wa sasa wa jimbo hilo.

Utafiti kutoka ndani ya CCM Bunda linadhihirisha kuwa kundi hilo ni la kada  mmoja wa CCM aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo ambapo katika mchakato wa kura za maoni wa mwaka 2010 alikuwa mpinzani mkali wa Bw. Kangi.

Hata hivyo Bw. Kangi naye licha ya umahiri wake wa kisiasa aidha anaonekana kuzidiwa kete na kundi pinzani ama hajataka kukaa nao meza moja kufanya suluhu kwa maslahi ya jamii yake.

Kuvuja kwa pakacha ni nafuu ya mchukuzi, au wapiganapo mafahali wawili ziumiazo ni nyasi, ugomvi wa Mwibara ni nafuu kwa jimbo la Bunda wakati jamii ya kawaida wa jimbo la Mwibara wakiumia.

Hainiingii akilini kupinga maendeleo ya eneo lako kwa kigezo cha chuki ya masuala ya siasa hii sasa imevuka siasa na kuingia ulimbukeni.

Inakuwaje watu wanapinga maendeleo yanayofanywa na mbunge wa jimbo hilo katika jimbo lao eti kwa sababu hawamtaki wakati kama ni madai ya kupata ubunge kwa rushwa kesi bado inaendelea mahakamani na maamuzi yatatolewa.

Hivi karibuni moja ya basi inayodaiwa kumilikiwa na Bw.Kangi ilipigwa mawe katika eneo la Nansimo jimboni humo likiwa limebeba baadhi ya wachezaji wa mpira kwenda Kisorya.

Naamini kwamba jimbo la Mwibara katika wilaya ya Bunda ni jimbo linaloongoza kwa kuwa na wasomi ambao nisingetegemea kuona chuki zao zikivuka mpaka kiasi hiki.

Wapo watu wenye busara ambao wanaweza kukaa chini na kufanya tathmini ya siasa ya Mwibara na kuleta pamoja makundi yanayozozana na kuunda Mwibara wenye nguvu.

Historia ya uongozi wa Mwibara hasa wabunge imejaa visasi bila kujali chama cha siasa wanachotoka wabunge hao, hii ni hatari.

Ni rai yangu kuwaomba wasomi wa kada mbalimbali kutoka Mwibara kukaa chini na kuona ni jinsi gani wanavyoweza kuivusha Mwibara kutoka katika ulimbukeni huu.

Bw. Mukama anaweza  kutumia ushawishi wake pia kurejesha umoja wa CCM jimboni Mwibara kwa maana kuwa chuki hii ikivuka mpaka itafikia hatua ya kurushiana risasi.

Tunatarajia kuuona Mwibara usio kuwa na chuki na mgawanyiko katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 bila kujali itikadi za vyama vya siasa.

0754569912


No comments:

Post a Comment