01 October 2012
Watakiwa kuuza pikipiki zikiwa na kofia mbili
Na Stella Aron
WAFANYABIASHARA wa pikipiki wametakiwa kuuza pikipiki zikiwa na kofia mbili ngumu ili kuwasaidia kupunguza majeraha kwa abiria pindi wanapopata ajali.
Agizo hilo limetolewa juzi Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam Bw.Elifadhili Mgonja kwenye ufungaji wa mafunzo ya waendesha pikipiki 200 yaliyofanyika mkoani humo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Usafiri (SUMATRA) Bw.Ahmed Kilima.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa uuzaji wa kofia hizo mbili utasaidia kupunguza majera kwa abiria na hata kusaidia watu kupoteza maisha.
Alisema kuwa sababu ya mafunzo hayo ni kutokana na hivi sasa pikipiki kuruhusiwa kubeba abiria huku madereva wengi wakiwa hawana elimu ya usalama barabarani sababu nyingine ni kuongezeka kwa idadi ya vifo vinavyotokana na pikipiki ambapo mwaka jana watu 945 wamekufa kwa ajali ya pikipiki.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Bw. Mohamed Mpinga, alisema kuwa kikosi chake kimeazimia kutoa mafunzo kwa madereva 8000 kwa nchi nzima hadi kufikia Desemba mwaka huu.
"Tunawaombe madereva mliopata mafunzo leo na kutunukiwa vyeti mheshimu sheria za usalama barabarani na muache kupita pindi taa nyekundu zinapowaka, " alisema.
Naye mkurugenzi wa SUMATRA Bw. Kilima alisema kuwa Serikali kwa kuzingatia kuwa maeneo mengi ya mijini na vijijini hayafiki kwa magari ilikubali kupitia kufanya marekebesho ili kuboresha usafiri nchini.
Mkurugenzi huyo aliwataka wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata na kuacha kupakia abiria zaidi ya mmoja kwani usafiri wa namna hiyo usiposimamiwa imara unaweza kuwa janga katika nchi.
mwisho
idadi ya watu wanaoumia pindi wanapopanda pikipiki hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment