01 October 2012

Wasomi watakiwa kujenga uzalendo nchini mwao



Na Daud Magesa,
Mwanza

WASOMI nchini wametakiwa kuwa waadilifu na kujenga uzalendo ili kulikwamua taifa na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali husani elimu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhasibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Bw.Noel Mtekateka, katika mahafali ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Mkolani Wilaya ya Nyamagana Jijini hapa.

Alisema wasomi na hasa vijana wakiwa na uzalendo na nchi yao, kwa kutumia elimu waliyoipata watasaidia kuleta maendeleo katika jamii na kukuza na kuimairisha uchumi wa nchi.

Bw.Mtekateka mwenye Digrii mbili katika masuala ya hesabu (Uhasibu),alisema hatarajii vijana wasomi wabaki kulalamika barabarani na kushiriki migomo isiyo na tija, jambo linaloipa serikali wakati mgumu na kushindwa kuwahudumia wananchi wake.

“Ni jambo la kusikitisha kuona vijana wanajiingiza kwenye migomo na vurugu zisizo na tija kwa Taifa.Hali hii inaipa kazi ngumu serikali badala ya kuhudumia wananchi inafikiria namna ya kutatua migogoro na migomo kama ya walimu na madaktari,lakini pia migomo hiyo inatuathiri sisi wananchi,”alisema.

Aliwataka vijana na wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kusaidia jamii na kujiepusha na vitendo vya ufisadi kwa kujenga uzalendo na wenye maadili Taifa liweze kupiga hatua.

“Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limerejea tena, uchumi ukiimarika litakuwa katika mstari na vijana wengi watapaswa kupitia huko wajenge uzalendo kwa nchi yao na kuitangaza na kuinua uchumi,”alisema Bw.Mtekateka.

Aliwaonya vijana hao kuwakataa wale wote wanaohamasisha vurugu na migomo ili kujenga taifa lenye amani na ustawi kwa kutumia elimu yao,badala ya kualalamika hovyo barabarani.

Awali Mkuu wa Shule hiyo ,Bw.Asencio Mathias, alimweleza mgeni rasmi kuwa baadhi ya wanafunzi nidhamu yao haikuwa nzuri ingawa walijitahidi kuwabadilisha mienendo yao na kuomba wazazi kusaidiana na walimu ili kujenga watoto kimaadili na nidhamu.


“Vijana hawa wanaohitmu leo wana mienendo tofauti,tumejitahidi kuwarekebisha na kuwa wenye maadili.Wenye mienendo safi watafanya vizuri katika masomo yao,lakini wenye tabia mbaya,watabaki kuwa wabangaizaji na wa madarasa ya chini wajiepushe na tabia hizo,”alisema Bw.Mathias.

Jumla ya wanafunzi 212 walihitimu masomo yao kati ya 230,ambapo wanafunzi 38 walishindwakuhitimu kutokana na matatizo mablimbali ikiwemo utoro, ujauzito na kuhama bila taarifa.

Shule ya Mkolani yenye kidato cha kwanza hadi cha sita inafundisha michepuo ya Sayansi, Biashara na  Sanaa,katika mitihani ya taifa mwaka jana ilishika nafasi ya 808 kitaifa kati ya shule 3,108,wakati kimkoa ilishika nafasi ya 88 kati ya  shule 251 za mkoa wa Mwanza.


No comments:

Post a Comment