05 October 2012

Wanaorubuni wanachama CCM sasa waonywa



Na Florah Temba, Moshi

CHAMA Cha mapinduzi (CCM), mkoani Kilimanjaro, kimewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho, kuacha kuwarubuni wanachama kwa kuwapa rushwa ili waweze kuchaguliwa kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.

Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Bw. Steven Kazidi, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho mkoani humo.

Alisema CCM hakipo tayari kufumbia macho vitendo vya rushwa katika uchaguzi zake ambapo mgombea yeyote atakayebainika kushinda kwa kutoa rushwa, ataadhibiwa kwa kanuni za chama.

“Rushwa inachangia kupatikana viongozi wasio waadilifu lakini kama tutambaini mgombea aliyetoa rushwa, atapokwa ushindi wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

“Natoa wito kwa wagombea wote mkoani hapa, waache kutoa rushwa ili wachaguliwe kihalali kwani katiba ya chama hairuhusu vitendo hivyo,” alisema Bw. Kazidi.

Aliwataka wanachama wa CCM kuchagua viongozi waadilifu, waaminifu na wachapakazi ambao watakijenga chama hicho badala ya kukibomoa na kuhakikisha wagombea wanaohitaji madaraka kwa kutumia rushwa hawapewi uongozi.

No comments:

Post a Comment