05 October 2012
Kero ya wanafunzi Eckernford Tanga ipatiwe ufumbuzi
VYOMBO vya habari, jana viliripoti maandamano yaliyofanywa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Eckernford iliyopo jijini Tanga.
Wanafunzi hao wanadaiwa kuandamana hadi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa halhashauri ya jiji hilo ili kupinga kitendo cha walimu shuleni hapo kutoingia darasani zaidi ya wiki moja.
Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa na mgomo wa walimu ambao hawajalipwa mishahara yao na mmiliki wa shule hiyo.
Kabla ya kuandamana, wanafunzi hao wanadaiwa kuvunja mali za ofisi shuleni hapo ili kuonesha hasira zao baada ya kuzuiwa kumuona Mkurugenzi wa Taasisi ya Eckernford.
Sisi tunasema, wanafunzi hao wanahaki ya kuandamana ili kudai haki ya kufundishwa na walimu hasa kwa kuzingatia kuwa, hakuna wanachodaiwa na uongozi wa taasisi hiyo lakini hatuungi mkono vurugu walizofanya na kuharibu mali za taasisi hiyo.
Ukweli ni kwamba, wanafunzi hao wamelipa ada ya mwaka mzima ili wapate elimu bora na pale wanaposhindwa kulipa kwa wakati, uongozi wa shule huwarudisha nyumbani.
Tumeshuhudia katika baadhi ya shule za sekondari wanafunzi wakirudishwa nyumbani baada ya kushindwa kulipa ada na michango mingine.
Upo umuhimu mkubwa wa uongozi wa Mkoa wa Tanga kuingilia kati sakata la wanafunzi hao kuhakikisha taasisi inayomiliki shule hiyo, inawalipa walimu ili waweze kuingia madarasani.
Elimu bora ni uti wa mgongo katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia ndiyo maana nchi mbalimbali duniani zimewekeza katika elimu ili jamii kubwa isome na kuitumia elimu waliyonayo kwenye harakati za maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii.
Taifa ambalo lipo nyuma kielimu, linakabiliwa na hali ngumu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali hivyo ni wajibu wa wanafunzi shuleni hapo kuhakikisha wanapata elimu bora ambayo itakidhi mahitaji yao na pale wanapoikosa lazima waipiganie.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment