05 October 2012
Mwakyembe awabeza wanaomkosoa
Na Mariam Mziwanda
WAZIRI wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, amewabeza watu wanaokosoa juhudi anazozichukua ili kuboresha miradi na taasisi za Wizara yake akidai watu hao wataendelea kuimba
ngonjera kutokana na elimu yao duni ya darasa la saba.
Alisema Wizara hiyo itaendelea kuongeza ufanisi wa kazi za maendeleo nchini na hakuna mradi usiotekelezeka kimkataba.
Dkt. Mwakyembe aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kumalizika Mkutano wa Pili wa Nchi za Afrika, ambao unajadili mfumo na utaratibu wa vifaa vya uhakika vinavyosababisha uwepo wa bidhaa bora kwa mlaji.
“Mimi kwa elimu niliyonayo siwezi kubishana na wasio na elimu ambao kila kukicha wanaangalia nimefanya kitu gani cha mandeleo ili wapotoshe ukweli, nitaendelea kufanya kazi na kuwaacha waendelee kutumia elimu zao za darasa la saba kutunga ngonjera.
“Watu wanaobeza maendeleo waelewe chini ya Wizara yangu hakuna mradi usiotekelezeka kimkataba ili kuondoa utendaji ambao ulizoeleka, mikataba itambana kila mmoja kukamilisha mradi kwa wakati,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Kutokana na hali hiyo, alisema Wizara hiyo ililazimika kufanya ziara katika Mamlaka ya Bandari nchini ili kujua kilichokwamisha mradi wa boya la mafuta kwa wakati hali ambayo imezaa matunda ambapo mradi huo utaanza kazi Novemba mwaka huu.
Alisema kukamilika kwa boya hilo, kutashusha bei ya mafuta na kudhibiti mfumuko wa bei nchini kutokana na ongezeko la kasi ya upakuaji na ushushaji mafuta bandari.
Aliongeza kuwa, meli ya kwanza itashusha tani 150 na kufungua njia ya kushusha na kupakia meli nne kwa mwezi hivyo kuondoa msongamano unaojitokeza mara kwa mara.
Akizungumzia mikakati ya Serikali kupitia mkutano huo, Dkt. Mwakyembe alisema Tanzania imejipanga kuboresha huduma
za reli hivyo ndani ya miezi sita ijayo, nchi za Afrika na Watanzania watarajie huduma bora za uhakika ili kuboresha uzalishaji.
“Mikakati hii ya Serikali inakwenda sambambana na njia zaidi za uboreshaji ugavi katika mazao ya chakula ili kukabiliana na tatizo la njaa na hatimaye kuwa na chakula cha kutosha,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji nchini Bw. Zacharia Mganilwa, alisema lengo la mkutano huo ambao Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji ni kupata uzoefu wa kiutafiti ili kukabiliana na maafa ya vifaa vya uzalishaji.
Alisema kupitia mkutano huo ambao umeshirikisha wawakilishi kutoka nchi za Ujerumani, Japan, Ufaransa, Marekani na Uingireza nchi za Afrika, waatabaini namna ya kuwafikia wahanga katika huduma bora za bidhaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment