02 October 2012

Waliojenga maeneo yasiyo rasmi nyumba zao kuvunjwa



Na Salim Nyomolelo

SERIKALI imesema nyumba zote zilizojengwa maeneo ambayo si rasmi zitavunjwa bila ya kuangalia thamani yake kama watabiani zimejengwa bila kwa kukiuka sheria na taratibu.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyum,ba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Goodluck Ole Medeye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani.

Alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua watu waliokiuka sheria na kujenga maeneo ambayo hayakupaswa kujengwa makazi ya watu hivyo nyumba hizo zitavunjwa.

Aliongeza kuwa, moja ya changamoto zinazoikabili Wizara hiyo ni uvamizi wa maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya huduma za jamii ambazo ili ziweze kutekelezwa, lazima Serikali ivunje nyumba zote zilizojengwa maeneo yasiyo rasmi.

“Miongoni mwa changamoto zinazoikabili nchi yetu kwa sasa ni usimamizi mbovu wa sheria ya mipango miji, vijiji, matumizi ya ardhi na ukosefu wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa makazi bora na mipango miji,” alisema.

Alisema maeneo ya Sinza na Mbezi Beach, Dar es Salaam,  yamepangwa lakini baadhi ya wananchi wanabadirisha matumizi ya ardhi kwa kuvamia maeneo ya wazi na kujenga makazi kiholela bila ya kibali.

Bw. Medeye alizitaka halmashauri zote nchini kusimamia sheria za mipango miji na kuwachukulia hatua wote ambao watakaozikiuka.

Akizungumzia kuhusu siku ya makazi duniani Bw. Medeye alisema asilimia 70 ya wakazi wote waishio mijini wanakaa katika makazi yasiyopimwa na ukosefu wa miundombinu.

Alisema Serikali inatekeleza utaratibu ya kuyatambua makazi yasiyopimwa na kuandaa utaratibu wa kuyapima, kuyaboresha, kuweka miundombinu ya msingi na kutoa hati miliki.

Aliongeza kuwa, katika jiji la Dar es Salaam miliki za viwanja 221,443 kati ya 400,000 zimeshatambuliwa na wamiliki 93,000 wamepewa leseni za makazi.



No comments:

Post a Comment