01 October 2012

UN yaipongeza Tanzania kwa kupeleka askari polisi Darfur


Na Mwandishi Maalumu

TANZANIA imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa nchi zilizoitikia vyema wito wa kupeleka idadi kubwa ya askari polisi wanawake kushiriki Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa (UN), katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.


Pongezi hizo zimetolewa jana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Polisi Kamishna, Ann-Marie Orler, ambaye pia ni Mshauri wa Polisi katika  Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa (DPKO).

Kamishna Orler aliyasema hayo katika barua yake kwa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania ina asilimia 33 ya askari wanawake waliopo katika operesheni za ulinzi wa amani.

“Kumbukumbu zetu zinaonesha Tanzania hadi sasa imepita lengo la UN la askari wanawake na wanaume kushiriki operesheni za ulinzi wa amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, ambalo limekuwa kwenye mgogoro na machafuko ya muda mrefu.

“Jimbo hili linahudumiwa na Jeshi la Mseto ambalo linajumuisha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika maarufu UNAMID,” alisema Kamishna Orler.

Aliongeza kuwa, Katibu Mkuu wa UN, Bw. Ban Ki Moon ameweka lengo la kuhakikisha hadi mwaka 2014, askari polisi wanawake wanaohudumu katika operesheni hizo wanafikie asilimia 20.

Alisema lengo hilo linawiana na azimio namba 1325 la Baraza Kuu la Usalama la UM, kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ambalo linazungumzia kwa kina athari wazipatazo wanawake na watoto wa kike kwenye nchi zenye vita au yanapotokea machafuko. 

Kamanda Orler alisema azimio hilo linatambua kuwa ni muhimu kuwepo na taasisi madhubuti ambazo zitawahakikishia wanawake  ulinzi, ushiriki wao katika mchakato wa kutafuta amani, kuchangia ujenzi na uhamasishaji ulinzi na amani ya kimataifa.

Alisema ili kuhakikisha ulinzi na mahitaji muhimu ya wanawake yanawakilishwa vyema ndani ya Polisi wa Umoja wa Mataifa, UM, limemtaka Bw. Moon kupanua majukumu, mchango wa wanawake katika maeneo yenye vita na machafuko.

“Ili kukidhi lengo la UM kuwa na asilimia 20 ya askari polisi wanawake, nchi wanachama zinatoa askari wake kushiriki katika operesheni za ulinzi wa amani.

“Nchi husika zinapaswa kuhakikisha usaili wanaoufanya angalau asilimia 50 ya polisi wanaochaguliwa wawe wanawake, polisi wa Tanzania walianza kushiriki katika operesheni hizi mwaka 2005.

“Walipeleka maofisa wachache nchini Angola, Sudani ya Kusini na Siera Leone, hadi sasa askari polisi zaidi ya 207 wakiwamo maofisa na wakaguzi, tayari wameshiriki katika operesheni hizi na wengine 187 wanasubiri kwenda Darfur na watatu Sudani ya Kusini,” alisema.

No comments:

Post a Comment