01 October 2012
Mwinyi: Viongozi tekelezeni wajibu wenu kwa jamii
Na Charles Lucas
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, amewataka viongozi kutekeleza wajibu wao kikamilifu ili jamii iweze kutambua mchango wao hasa vijana ambao wengi wao hawana ajira hivyo kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Bw. Mwinyi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizindua mkakati wa wakazi wa Kata ya Kwadelo, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma wenye lengo la kuwarudisha nyumbani vijana waishio Dar es Salaam ili waweze kujishughulisha na kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza na kuleta mapinduzi ya kijani.
Alimpongeza Diwani wa kata hiyo, Alhaj Omary Kaliati, kutokana na juhudi zake za kuwasaidia vijana na kuhamasisha maendeleo ili jamii iweze kuondokana na umaskini.
“Nimefurahishwa na mikakati ya maendeleo inayofanywa na Alhaj Kaliati, naomba aungwe mkono kwa kupewa ushirikiano katika juhudi zake ili atokomeze umaskini katika jamii,” alisema.
Alisema awali Alhaj Kaliati alimfuata ili aweze kukabidhi baadhi ya matrekta lakini bado aliongeza mengine ambayo hivi sasa yanatumika kwa shughuli za kilimo.
Bw. Mwinyi alikabidhi matangi ya maji na kitanda maalumu cha kujifungulia wajawazito ambapo misaada hiyo ilitolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe kwa wakazi wa kata hiyo.
Kwa upande wake, Bw. Kaliati alisema wameiabi vijana wengi wan nia ya kufanya shughuli za kilimo lakini walikosa ushikishaji hivyo lengo lake ni kuhakikisha kila kijana anakabidhiwa hekari tano ambazo atazilima na trekta kwa mkopo ambao utarejeshwa katika kipindi cha mavuno kila hekari sh. 30,000.
Mmoja wa Vijana walijiunga na mpango huo, Bw. Mashaka Ramadhani, alisema wapo tayari kushiriki katika mkakati huo kwani vijana wengi huondoka vijijini na kukimbilia mjini kwa sababu ya kukosa uwezeshaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment