01 October 2012

TEC: Urasimu bandari za Tanzania umewakimbiza wafanyabiashara


Na Mwandishi Wetu

SABABU kubwa inayochangia wafanyabiashara kuacha kuitumia bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ili kuingiza mizigo yao ni urasimu unaodaiwa kufanywa na maofisa forodha wanaohusika na ushuru wa kodi ya mapato kwa wafanyabishara wanaopaswa kulipia kodi hiyo Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Mwenyekiti wa Baraza la Uchumi mkoani Tanga (TEC), Bw. Abraham Lukindo, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya wajumbe wa baraza hilo kufanya ziara maalumu katika Bandari ya Mombasa, nchini Kenya.

Lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na wafanyabiashara wanaotumia bandari hiyo wakiwemo Watanzania ili kujua sababu iliyowafanya washindwe kuingiza mizigo yao katika bandari zilizopo nchini.

Alisema wafanyabiashara hao wanalalamikia kitendo cha maofisa wa forodha katika bandari husika kuchelewesha nyaraka zao na kusababisha wapoteze muda mwingi hadi kupata mizigo yao.

“Bandari ya Mombasa hakuna urasimu, maofisa wao wanajali muda ili wafanye biashara ndio maana sisi wafanyabiashara wa Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Malawi na Zambia tunalazimika kutumia bandari yao kuingiza mizigo yetu.

“Gari unazoziona nazipeleka Songea, ni bora kutolea magari Mombasa au Msumbiji kuliko nyumbani Tanzania, ambako siku nne hazitoshi kutoa magari hata kama nyaraka zote ziko sawa na haziitaji marekebisho yoyote,” alisema mfanyabiashara kutoka mjini Mbeya, Bw. Mwalubandu Said.

Aliongeza kuwa, ili Tanzania iweze kupiga hatua katika eneo hilo lazima ifanye mabadiliko ya makusudi katika muda na ushuru wa forodha na kama Serikali itaweza kufanya mapinduzi hayo, wafanyabiashara wataanza kurudi kama ilivyokuwa zamani.

“Sisi tunaamini kuna mambo ya makusudi yanyofanywa na maofisa wa forodha kuua uchumi wa Tanzania kupitia baadhi ya wafanyakazi serikalini.

“Kama viongozi wa Serikali yetu watashindwa kuzingatia ushauri huu, wafanyabiashara wa Watanzania wataendelea kuingiza mizingo yao katika bandari ya Mombasa, Msumbiji na Malawi,” alisema Bw. Said.

No comments:

Post a Comment