28 September 2012

Mchujo CCM waibua mapya *Baadhi ya wagombea wadaiwa kukosa sifa *Nape amtetea Makamba, Wassira atoa neno



Kassim Mahege na Stella Aron

SIKU mbili baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumalizika kikao chake cha  Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), mjini Dodoma, mambo mapya yamezidi kuibuka.

Inaelezwa kuwa, wapo baadhi ya vigogo ndani ya CCM ambao majina yao yalipitishwa kwenye mchujo wakidaiwa kukosa sifa pamoja na uwezo mdogo wa kukitumikia chama hicho.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili, zinasema baada ya mtandao wa vigogo hao kupenya katika mchujo huo, hivi sasa wameanza kujipanga bila kujali uwezo wao wa kukisaidia chama.

Habari zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali mjini Dodoma na Dar es Salaam, zilidai mtandao huo uliokuwa umejipanga kuhakikisha majina yao yanapita katika mchujo huo.

Vyanzo hivyo viliongeza kuwa, mtandao huo ulikuwa ukipigiwa debe na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba.

Kutokana na madai hayo, gazeti hili lilimtafuta Bw. Makamba, ambaye alisema yeye si msemaji wa tuhuma hizo bali atafutwe Katibu Mkuu wa sasa Bw. Wilson Mukama au Katibu wa Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye.

“Unamfahamu katibu wa CCM, Bw.Mukama, yeye ndiye msemaji wa chama, kwanini unawasumbua wastaafu waliopumzika?” alihoji Bw. Makamba na kusisitiza anayestahili kuulizwa juu ya tuhuma zinazomkabili ni Bw. Mukama.

Akizungumzia madai hayo, Bw. Nnauye alisema madai hayo ni ya kipuuzi na wanaoyatoa wana uelewa mdogo.

“Ni upuuzi mtupu, Makamba ni mtu mmoja na maamuzi yamefanywa na kikao, wanaotoa madai hayo ni watu wenye akili ndogo andika hivyo,” alisema Bw. Nnauye.

Aliongeza kuwa, kikao kilichopitisha majina hayo kilikuwa na wajumbe zaidi ya 200, hivyo ni jambo la kushangaza mtu anaposema Bw. Makamba ameingiza watu wake wasio na sifa.

Akizungumzia hoja iliyoibua mjadala ya kuwapumzisha wazee na kuwapa nafasi vijana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira, alisema uamuzi huo ni mzuri.

“Mimi sioni makosa yoyote kwa sababu chama chochote cha siasa lazima kiwe na watu wa kurithi, hata katika familia lazima awepo mtu wa kurithi na kuiongoza familia.

“Utamaduni huu haupo kwa CCM pekee, chama ambacho kinaandaa vijana hakuna tatizo na duniani kote wanafanya hivyo,” alisema.

Akizungumzia madai ya kuendelea kupewa nafasi za kukitumikia chama kutokana na umri wake kuwa mkubwa, Bw. Wassira alisema “Wapo kaka zangu ambao umri wao mkubwa kuliko mimi kule NEC, mbona hawaulizwi?

“Jambo la msingi hapa ni kuangalia uwezo wa kufanya kazi si umri, tutafanya maamuzi kutokana na uwezo wa mtu,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa, mambo ya kuzingatia katika ufanisi ni matatu ambayo ni uzalendo, uwezo wa kufanya kazi na uadilifu sio umri.

“Mimi nimezaliwa mwishoni mwa 1945, lakini ndani ya NEC kuna wajumbe ambao wamezaliwa kabla ya 1940, kwanini niangaliwe mimi tu, inakuwaje,” alihoji Bw. Wassira.

Alisema kitu muhimu ni kukubalika katika jamii nduio maana hakuna lawama zozote alizopewa na kuongeza kuwa, lazima vijana waandaliwe kwa ajili ya kukitumia chama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, alionekana kukerwa na hatua CCM ya kuwaondoa wazee na kuweka vijana akidai njia hiyo si sahihi na haiwezi kufanikiwa kiuongozi.

Alisema kiongozi mzuri ni yule aliyeandaliwa si wa kuokotwa jalalani hivyo kusababisha kukosa uadilifu na ufisadi.

No comments:

Post a Comment