08 October 2012
Simba hadi raha *Yaichapa JKT Oljoro 4-1 *Yanga kazi ipo leo Kagera
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba, imeendeleza wimbi lake la ushindi baada ya jana kuichapa JKT Oljoro ya Arusha, mabao 4-1 katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.
Mechi hiyo ilipigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, imeifanya Simba icheze mechi sita mfululio bila kufungwa na kufikisha pointi 16 huku Azam FC yenye pointi 13 ikishika nafasi ya pili.
Katika mechi hiyo, kiungo, Amr Kiemba aliibuka shujaa baada ya kuifungia Simba mabao mawili na mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Emmanuel Okwi akifunga moja na lingine lilifungwa na Felix Sunzu kwa mkwaju wa penalti na bao la kufutia machozi la JKT lilifungwa na Paulo Nonga.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi kwa kila timu kufanya mashambulizi langoni mwa mpinzani wake lakini Simba ilikuwa ya kwanza kubisha hodi dakika ya nne baada ya Felix Sunzu kupiga shuti lililotoka sentimeta chache langoni mwa JKT.
JKT ilijibu shambulizi hilo dakika ya 12 kupitia kwa Nonga ambaye alipiga kichwa kilichotoka nje ya goli akiunganisha krosi ya Meshack Nyambele.
Baada ya timu hizo kushambuliana kwa zamu, Kiemba aliwainua mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao dakika ya 16 akiunganisha krosi iliyopigwa na Edward Christopher ambaye alifanya kazi nzuri ya kumpiga chenga beki, Nato Zubeiry na kumpasia mfungaji.
Bao hilo, liliwazindua usingizini JKT ambao walianza kuliandama lango la Simba na dakika ya 29, Nonga aliisawazishia timu yake kutokana na makosa yaliyofanywa na beki Juma Nyosso kwa kushindwa kumzuia kupiga shuti ambalo lilizama moja kwa moja wavuni huku kipa, Juma Kaseja akiruka bila mafanikio.
Mashabiki wa timu zote wakiamini timu hizo zitakwenda kupumzika zikiwa zimefungana bao 1-1,lakini Kiemba aliwabadili mawazo mashabiki hao kwa kufunga bao la pili kwa kichwa ikiwa ni dakika moja kabla ya mapumziko akiunganisha krosi ya Nassor Said 'Chollo'.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko ambapo Christopher alitoka na kuingia Haruna Moshi 'Boban', Paulo Ngalemwa alitoka na kuingia Kigi Makasi na Jonas Mkude nafasi yake ilichukuliwa na Daniel Akuffor.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda ambapo dakika ya 82, Okwi aliifungia Simba bao la tatu na baadaye alipewa kadi ya njano baada ya kushangilia bao hilo kwa kuvua jezi.
Ikiwa imebaki dakika moja kabla kipyenga cha mwisho kupulizwa, Sunzu lihitimisha kalamu hiyo ya mabao kwa kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
Katika mechi hiyo, JKT, ilipata pigo baada ya mchezaji wake, Nyambele kuoneshwa kadi ya pili ya njano baada ya kumchezea faulo Boban.
Naye Mwandishi, Daudi Magessa kutoka Mwanza, anaripoti kwamba, wenyeji Toto African ya jiji humo, imetoka kifua mbele baaada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1 katika mechezo uliopigwa Uwanja wa CCM, Kirumba.
Mabao ya Toto yalifungwa na Severin Costantine dakika ya 13 na Selemani Kibuta dakika ya 64 baada ya kuonana vizuri na Emmanuel Swita na lile la JKT lilifungwa na Amosi Mgisa dakika ya 32.
Naye Mwandishi Wetu, Rashidi Mkwinda kutoka Mbeya, anaripoti kwamba timu ya Prisons, imeshindwa kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine baada ya kulazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mechi hiyo ilikuwa na ushindani wa aina yake kutokana na timu zote kucheza soka safi na la kuvutia.
Matokeo mengine ya ligi hiyo ni kwamba, Mgambo Shooting ya Tanga imeichapa Polisi Morogoro bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera ambapo wenyeji, Kagera Sugar itaikaribisha Yanga katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.
Mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa jana lakini ilisogezwa mbele kutokana na uwanja huo kuwa na shughuli zingine za kijamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment