02 October 2012
Sheria ya usafi wa mazingira itekelezwe kivitendo
Na Stella Aron
"USAFI wa mazingira ni jukumu letu sote, ni suala muhimu kwa afya na uhai wetu,"
Kauli hiyo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na viongozi mbalimbali nchini kwa nia ya kuhakikisha kuwa jamii inafuata kanuni za usafi wa mazingira nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mohammed Gharib Bilal alizindua kampeni ya usafi wa miji na majiji na kuziagiza Halmashauri za Manispaa, Miji na Majiji kuhakikisha kuwa kampeni hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa ukamilifu ili kutimiza malengo yaliyowekwa
Katika uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam Dkt. Bilal alitumia nafasi hiyo kwa kuziagiza kujipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa kampeni hiyo inatekelezwa kwa ufanisi unaotarajiwa na kuahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kampeni hiyo kote nchini.
Dkt.Bilal anasema kuwa usafi si wa kiwango cha kuridhisha hivyo kusababisha madhara makubwa ya kiafya, kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa majiji na miji nchini.
Anasema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya magonjwa yanayotibiwa katika vituo vya afya nchini yanahusiana na uchafuzi wa maji na mazingira. Kwa maneno mengine hali mbaya ya usafi wa mazingira nchini inagharimu mno kiafya, kiuchumi na kijamii.
Aliyataja madhara mengine kuwa ni pamoja na kuathiri mandhari ya makaazi ya watu kutokana na kuzagaa ovyo kwa uchafu wa kila aina ukiwemo taka ngumu kama mifuko ya platiki, harufu mbaya inayotokana na kuoza kwa taka na maji machafu yanayotiririka ovyo.
Aliongeza kuwa taka ngumu hasa mifuko ya plastiki inachangia katika kuziba miundombinu ya mifereji ya maji ya mvua na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya miji yetu ambapo hali hiyo inatokana na dhahiri kuwa usimamizi mbovu katika usafi wa mazingira na kuchangia katika kudumaza jitihada za taifa za kupambana na umaskini na kuinua kiwango cha maisha cha Watanzania.
Katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Makamu wa Rais aliitangaza siku ya Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi kuwa itakuwa ndio siku ya usafi wa mazingira katika miji na majiji na ametoa wito kwa kila mwananchi kushiriki kikamilifu na kuiunga mkono kampeni hiyo ambayo itakuwa ikifanyika kuanzia saa moja hadi saa nne asubuhi.
Katika kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi kwa kushirikiana na ofisa usafirishaji wa manispaa hiyo Bw. Samwel Bubegwa pamoja na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu, Ukonga Bw. Wilfred Kipodya ambaye ni kati ya viongozi ambao wamepata mafanikio katika suala la usafi wa mazingira katika mtaa wake na kuwa mfano walizindua kampeni ya usafi.
Bw. Mushi anasema kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala hilo amelazimika kuungana na waandishi wa habari na kuzindua kampeni ya usafi wa mazingira katika wilaya hiyo na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wilaya hiyo inakuwa safi.
Anasema kuwa hali duni ya usafi wa mazingira katika miji na majiji kuwa inachagiwa pia na ukosefu wa miundombinu na nyenzo za kuzolea taka lakini na kuwafanya wasimamizi wa sekta hiyo kushindwa kufanikisha malengo yao.
Anasema ili manispaa hiyo iwe yenye kata 26 iwe safi wananchi wanashauriwa kuweka safi mazingira yao ikiwemo barabara, kuzoa taka, kufukia madimbwi ya maji, kuzibua mifereji na maji ya mvua, kufukia makorongo, kupanda nyasi na miti pamoja na kuelimisha na kuhamaisisha jamii juu ya usafi wa mazingira.
Ofisa usafirishaji Bw.Bubegwa aliwataka wananchi kuzingatia kwa makini usafi wa mazingira pamoja na kushiriki kikamilifu katika ulipaji wa taka unaofanywa na baadhi ya vikundi ama taasisi.
Anasema kuwa Manispaa ya Ilala imekuwa ikizalisha taka kwa siku tani 1088 za majumbani huku zinazozotolewa ni asilimia 55 tu na kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
"Asilimia 70 ya makazi ya watu hayafikiki kirahisi hivyo hulazimika kubebwa kwa namna mbalimbali kutokana na maeneo hayo yasiyopimwa ili manispaa hiyo kuwa safi, " anasema.
Bw. Bubegwa anasema kuwa kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa taka hizo kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wakazi kushindwa kuchangia uzoaji wa taka, uwezo mdogo wa baadhi ya wakandarasi.
Hata hivyo anasema kuwa ili suala la usafi wa mazingira liweze kudumu ni bora sasa sheria ya usafi wa mazingira likawekwa msisitizo kwa ulipaji wa fani ya papo kwa hapo kwa kila mkazi anayekamatwa akitupa uchafu katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Anasema kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo bado wanasiasa hawana uelewa mpana zaidi kuhusiana na suala la afya na kusababisha kuwepo kwa gharama kubwa za uondoshaji wa taka katika maeneo mbalimbali ndani ya manispaa hiyo.
Anaongeza kuwa asilimia 70 ya magonjwa yanayotibiwa katika vituoi vya afya hutokana na uchafu kutokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu kuhusu afya.
Anasema kuwa ili kudhibiti mazingira ya manispaa hiyo kuwa safi ni bora sasa adhabu ya faini ya sh. 50,000 kwa atakayekamatwa kwa suala la utupaji taka ama kesi inayotokana na mazingira na pia kifungo cha adhabu ya kwenda jela miezi 12 vitiliwe mkazo.
Akibainisha kuhusiana na sheria hiyo, mwanasheria wa manispaa hiyo Bi. Pamela Mugarula, anasema sheria za utupaji wa taka ovyo zipo na zinapaswa kutekelezwa.
Anasema ni kweli kumekuwa na tatizo la utekelezaji wa sheria hiyo lakini ni kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri unaozingatia sheria ili watuhumiwa waweze kufikishwa sehemu zinazostahili.
"Matumizi ya sheria ndogo ambazo zimetungwa mwaka 2011 kwa watu wanaozikiuka wakiwemo wanaogoma kulipa ada na kufafanua makosa, adhabu ikiwemo faini zitakazowakabili kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha sheria hizo," anasema.
Bw. Charles Wabura ni ofisa msimami wa taka ngumu katika manispaa hiyo, alisema kuwa tatizo la usafi wa mazingira linapaswa kushirikiana kikamilifu kati ya viongozi na wananchi.
Anasema kuwa bado manispaa hiyo inakabiliwa na uhaba wa magari ya uzoaji taka, uharibifu wa miundombinu na kusababisha kushindwa kufanyika kwa usafi, vifaa vya uzoaji taka, uchangiaji wa taka kwa baadhi ya wananchi na uwezo mdogo wa kuchangia.
Mwenyekiti wa mtaa wa Madafu Bw.Kipondya, anasema kuwa mtaa huo umepata mafanikio kutokana na kuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya wananchi na viongozi pamoja na kuwepo kwa vitendea kazi.
Anasema kuwa kutokana na mafanikio hayo amekuwa akipata misaada mbalimbali ya vifaa na kusaidia kuongeza kasi zaidi katika uzoaji taka na kupunguza kasi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko ambako mtaa huo ulikuwa ukisumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa kipindupindu mara kwa mara.
Hivi karibuni katika uzinduzi wa kampeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira Dkt.Teresia Huvisa aliwataka wananchi kuzingatia kwa makini usafi wa mazingira pamoja na kuepuka vitendo vya kujisaidia ovyo kwani vitendo hivyo vitasababisha kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo za kupigwa faini za hapo kwa papo na hata kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
“Ukijisaidia ovyo utakamatwa na kupigwa faini hapo hapo ya sh. 50,000 ukitema mate ovyo faini sh. 50,000 na ukitupa pasipo stahiki hata vocha ya simu iliyotumika utapigwa faini ya Sh.50,000 au hata kufikishwa mahakamani, ”anasisitiza katika uzinduzi huo.
Mazingira yanatakiwa kulindwa na kila mtu katika jamii kwani sehemu ya uhai wa kila kiumbe hai.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment