02 October 2012

Hamasa za kilimo ziende sanjari na upatikanaji pembejeo bora



Na Rashid Mkwinda

MVUA za Kwanza ni za kupandia," ilikuwa ni kauli mashuhuri enzi za Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, akihamasisha kilimo ambacho kwa wakati huo kilikuwa na kauli Mbiu ya ‘’Kilimo ni Uti wa Mgongo".


Hamasa hiyo zilikwenda sanjari na upatikanaji wa pembejeo rahisi za kilimo wakati huo ardhi ilikuwa bado haijakumbwa na uharibifu wa mazingira huku baadhi ya maeneo wananchi wakilima kwa kutumia mbolea ya asili huku wengine wakinufaika kwa kulima bila kutumia aina yoyote ya mbolea.

Kipindi hicho kila mmea uliopandwa ulimea na kukua vyema na wakulima walinufaika kwa mazao yao ingawa baadhi ya maeneo yalikumbwa na ukame kutokana na tabia nchi iliyotokana na majanga ya asili kama vile ukame uliosababisha kutonyesha mvua na mafuriko.

Hata hivyo kwa wale waliobahatika kulima hususani katika maeneo ya mikoa maarufu kwa kilimo cha mazao ya chakula kama vile Rukwa, Mbeya, Iringa na Ruvuma walibahatika kuvuna mazao mengi ingawa matatizo ya masoko kwa mazao ya biashara yalikuwa bado hayajapatiwa ufumbuzi kwa wakati huo.

Nilichokusudia kukiweka bayana katika makala haya juma hili ni kauli  ya hamasa iliyowataka wakulima kuzingatia kuwahi kupanda kwa mvua za mwanzo ambayo iliambatana na  maandalizi ya mashamba.

Kwa zama hizi kauli hizo zimepotea ama zimekufa kabisa kutokana na tatizo kubwa linalowakuta wakulima juu ya ukiritimba wa pembejeo za kilimo ambazo serikali kupitia mpango wake wa kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula iliamua kutenga ruzuku kwa wakulima nchini.

Suala la Pembejeo za kilimo limehamisha fikra za wakulima nchini ambapo tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo wa pembejeo kumekuwa na matatizo lukuki yanayowafanya wakulima wafikirie kuacha kilimo na kufanya shughuli zingine ambazo zitawawezesha kununua chakula.

Hali hiyo imekuja kutokana na ukweli kuwa ipo dosari katika ugawaji wa pembejeo za kilimo hususani mbolea ya ruzuku ilhali makampuni yanayozalisha mbegu bora yakikumbana na vikwazo vya mbegu zao kuchakachuliwa na wajanja wachache.

Ifahamike wazi kuwa suala la mbegu bora nchini ni miongoni mwa masuala nyeti ambayo hayana budi kuheshimiwa mbapo serikali kwa kuzingatia hilo iliona vyema kuunda sheria inayoweza kujitegemea namba 18 ya mwaka 2003 (Seeds Act no 18,2003) ambapo utekelezaji wa sheria hiyo kwa ukamilifu utasaidia kulinga usalama wa chakula nchini (Food Security).

Mbali na tatizo la pembejeo za kilimo lipo tatizo lingine ambalo kimsingi linatokana na kuchelewa mvua katika baadhi ya maeneo nchini kama vile Dodoma ambako kiasili kuna historia hiyo ya ukame kwa miaka mingi.

Athari katika maeneo yenye ukame hushamiri zaidi pale mvua inapochelewa kunyesha ambapo ardhi nyingine huanza kupasuka na kukauka na mara mvua inapoanza kunyesha husomba udongo na kufukia mazao yaliyopandwa katika maandalizi ya kauli mbiu ya Mvua za Kwanza ni za Kupandia.

Naamini nia ya wakulima ni kutekeleza kwa dhati dhana ya kilimo kwanza ambayo wanaamini kwa wakati huo ndilo linaloweza kuwa suluhisho na tiba inayoweza kulete tija katika kilimo bali matatizo sugu ya pembejeo na mbegu bora za kilimo na kutegemea mvua pekee badala ya kuwepo kwa mfumo wa umwagiliaji linaweza kuwa ni tatizo ambalo kamwe haliwezi kupatiwa ufumbuzi kwa miaka mingi ijayo.

Hivi sasa hivi upo mpango wa usambazaji wa Power Tiller na Trekta vijijini, ni mpango mzuri kutokana na ukweli kuwa kwa zama hizi matumizi ya jembe la mkono si rafiki tena wa kilimo bora cha kisasa, hata hivyo tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta unaweza kuwa ni mzigo mwingine kwa mkulima na hivyo kumsababisha mkulima akate tamaa ya kuendelea na kilimo.

Lipo jambo la kutafakari kwa kina ambalo linaweza kuwa ni suluhisho la kilimo na tija kwa wakulima nchini iwapo kutakuwa na mfumo bora na makini wa umwagiliaji bila kutegemea mvua.

Kinachoonekana hapa ni kwamba kama vile hakuna jitihada za dhati kwa serikali  kutengeneza mfumo wa umwagiliaji.

Kulingana na tabia fuatana na mabadiliko ya tabia nchi ni kujidanganya kutegemea kilimo cha mvua. Ni lazima kuingia katika mfumo wa umwagiliaji ingawa suala hili la Kilimo linaendelea kuwa ni kitendawili kisichopatiwa ufumbuzi na msimu wa kilimo ndio huo unakaribia.

Tunaweza kulia na hata kutoa machozi ya damu kuhusu matatizo yanayowakumba wakulima ambapo matatizo ya ukame yamekuwa kama wimbo ambalo ni sawa na  balaa  la kujitakia huku tatizo hilo likitupiwa kwa Mwenyezi Mungu ilhali ukweli ni kwamba inawezekana kabisa kukosekana kwa viongozi makini wenye upeo ndilo tatizo halisi.

Yapo mengi ambayo  hayatiliwi mkazo juu ya mkakati huu wa Kilimo kwanza kumkomboa mkulima wa chini, labda ni kutokana na sera ya kilimo ambayo imelenga kwa wawekezaji wakubwa wa kilimo na kuwaacha wakulima wadogo wakiendelea kuhaha kwa nia ya kujikomboa kupitia kilimo.

Serikali lazima ikubali kuwa lipo tatizo katika kuwasaidia wakulima katika nchi ambayo imesheheni ardhi yenye rutuba ambapo hata hivyo hakuna mipango na njia mbadala endelevu za  kuwafundisha wakulima njia bora za kuhifadhi mazao yao
ili yawe na ubora na ushindani katika  soko la dunia.

(rashidmkwinda@yahoo.com 0713-310096)









No comments:

Post a Comment