01 October 2012

Padri Mapunda akemea uongozi wa kupeana


Na Goodluck Hongo

PADRI wa Kanisa Katoliki nchini Baptiste Mapunda, amekemea tabia ya kupeana uongozi ndani ya familia akidai hali hiyo itakwamisha utendaji kazi wenye tija ili kuchochea maendeleo.

Alisema uongozi wa kupeana unaongeza pengo kati ya matajiri na maskini ambao unaongezeka siku hadi siku badala ya kupungua.

Padri Mapunda aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki lililopo Manzese, Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, viongozi ndio walioua Azimio la
Arusha ambalo lilianzishwa na hayati Mwalimu Juliuis Nyerere na kuligeuza kuwa azimio la wala rushwa na ufisadi.

Alisema hali ni mbaya kwani uongozi umekuwa wa kupeana kifamilia na kuongeza pengo kubwa la matajiri na masikini ambapo  kila kukicha umasikini unaongezeka badala ya kupungua.  

“Musa aliwaokoa wana wa Waizrael katika utumwa na sisi tusiwe na Ukristo wa mashaka, lazima tuhojiane kuhusu utajiri wetu kama umepatikana kwa njia halali au umetokana na uongozi wa kupeana ambao mtu akiiba anaachwa,” alisema Padri Mapunda.

Alisema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwenye kipaji akimfananisha na Musa kwani alitumia hekima na busara kuwaondoa Watanzania katika ukoloni.

Aliongeza kuwa, leo hii nchi inahitaji ukombozi wa pili kwani ule wa kwanza Mwalimu alijitahidi ukapatikana.

Padri Mapunda alisema kwa hali ilivyo sasa, watu wachache   wamejilimbikizia mali na wengine kutuhumiwa kuiba fedha za walipa kodi lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na wezi wa kuku ndio wanaofungwa jela.

Alisema viongozi ambao hawana wivu, chuki ndio wanaofanikiwa katika uongozi wao kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere ambaye hakuwa na makuu hadi alipoamua kuondoka madarakani.

Aliongeza kuwa, viongozi wengi waliopo sasa wana chuki pamoja na kuzuia vipaji vya wenzao ili waendelee kuwepo madarakani kitu ambacho ni hatari na kinalipeleka Taifa pabaya.

“Mwalimu alikuwa kiongozi bora, alitumia upole wake kuongoza nchi na hakutumia bunduki kuwaondoa wakoloni zaidi ya kuongoza kwa kufuata misingi ya haki na usawa, katika kipindi chake sijawahi kusikia walimu, madaktari wamegoma au mwandishi kuuwa,” alisema.

Aliwataka Wakristo kuona umuhimu wa kutoa maoni yao kwa tume iliyoundwa kuratibu mchakato wa Katiba Mpya bila kuingiza kipengele cha dini ambacho ni hatari.

“Jambo la msingi tuhakikishe Rais anapunguziwa madaraka na matumizi ya vyombo vya dola yasiwepo katika siasa, viongozi wengi hawakuchaguliwa kwa haki ndio maana Taifa limekuwa la majanga makubwa,” alisema Padri Mapunda.

No comments:

Post a Comment