01 October 2012

CCM ikimee visasi baada ya kumaliza chaguzi zake


HIVI sasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipo katika mchakato wa kufanikisha changuzi mbalimbali ndani ya chama hicho baada ya Kamati Kuu (CC), kupitisha majina ya wagombea mjini Dodoma.

Chaguzi hizo zinapewa umuhimu mkubwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kama sehemu ya maandalizi ya CCM kuendelea kushika dola katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Baadhi ya vyombo vya habari, vimeripoti kuwa katika maeneo mengi, wagombea wasio waadilifu wametumia uwezo wao wa kifedha kuwahonga wajumbe ili waweze kushinda nafasi walizogombea.

Kitendo hiki ni ukiukwaji mkubwa wa agizo la Rais Kikwete ambaye alisema, Serikali yake haipo tayari kuona baadhi ya wagombea wa nafasi za uongozi wananunua uongozi.

Rais Kikwete hakusita kusema kuwa, rushwa katika uchaguzi ni tatizo kubwa kwani baadhi ya wagombea wanalichukulia ni jambo la kawaida bila wapiga kura kujua madhara yake.

Sisi tunasema kuwa, wajumbe wenye dhamana ya kuchagua viongozi wanapaswa kutambua rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo ya wananchi.

Kama watapokea rushwa na kumpa uongozi mgombea asiye na sifa wala uwezo, atakuwa ameshiriki kuliangamiza Taifa na kukwamisha mikakati ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya chama tawala.

Jambo la msingi ni kuchagua wagombea wasiotoa rushwa kwa sababu wanajiamini kutokana na uwezo walionao kiutendaji ndio maana hawana hofu ya kuwatumukia wananchi wakiamini kama watapewa uongozi watawajibika ipasavyo kutatua kero.

Kimsingi wajumbe wenye dhamana ya kuchagua viongozi wanaweza kubadili mitazamo ya baadhi ya wanasiasa ambao wameathiriwa na utaratibu wa takrima.

Upo umuhimu wa CCM kukemea visasi na chuki za baadhi ya wagombea ambao kukosa kwao uongozi, kunaweza kukwamisha mikakati ya maendeleo kwa viongozi waliochaguliwa.

Visasi na chuki ndani ya chama ni kirusi hatari kinachoweza kuigombanisha Serikali iliyopo madarakani na wananchi kwa sababu ya hasira za wagombea husika kukosa uongozi ili wajinufaishe kwa masilahi binafsi.

Tukichagua viongozi makini, hawatatumia madaraka tuliyowapa kujinufaisha kwani rushwa inakuza maadili yaliyooza na mambo muhimu katika maisha ni ukweli, sheria na utu.

No comments:

Post a Comment