08 October 2012
Mchakato wa katiba mpya na ubovu wa sheria zetu
Na Debora Mushi
KATIKA nchi yoyote, mfumo wa kisheria ni muhimu sana katika kujadili na kuelewa haki mbalimbali zilizopokwa raia wake. Ni katika sheria za nchi ndipo wananchi wa makundi mbalimbali wanaweza kuelewa na kudai haki zao za kiraia na kibinadamu za kimsingi.
Sheria ni mhimili mkuu wa kutoa na kulinda maslahi na haki za raia ikiwa ni pamoja na mahusiano ya makundi mbalimbali katika jamii yoyote.
Tangu uhuru sheria za Mfumo wa sheria za Tanzania umepitia mabadiliko kadhaa. Hata hivyo, sheria zihusuzo masuala ya makuzi ya watoto, mazingira ya vijana na uzazi salama zimepata kupitiwa mara chache sana.
Kwa mfano, sheria ya ndoa ya mwaka 1971 haijawahi kufanyiwa mabadiliko au marekebisho makubwa katika miaka zaidi ya thelathini sasa. Kwa sababu hiyo baadhi ya watanzania wamekuwa wakilalamikia kupitwa kwake na wakati, na kufika kupingana kimantiki na utendaji wake na sheria zingine zinazohusu vijana, wasichana na haki za kimsingi za wanawake na watoto.
Imefika wakati sheria ya ndoa ya 1971 inapingana kimsingi na baadhi ya vipengele vya utoajihaki vilivyomo katika sheria za nchi ikiwemo kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), sheria ya makosa ya kujamiiana (1998) na sheria za Elimu (1978), Kazi na watoto ambazo zote zimetungwa baada ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Aidha tangu kutungwa kwa sheria ya ndoa mwaka1971, hakujawahi kufanyika marekebisho makubwa juu yake na sheria nyingine zinazohusiana nayo. Hata marekebisho mbalimbali katika katiba ya nchi tangu 1977 (yapatayo 14 hadi leo) hayajawahi kutoa mwanya wa kutazama maswala ya ndoa na uzazi salama kwa wanawake, watoto na vijanakama ambavyo ingepaswa iwe.
Hata hivyo pamoja na kuingia mikataba mbalimbali na jumuia za kimataifa katika kulinda haki, vijana na wanawake wameshuhudia matamshi tu katika mikataba hiyo bila utekelezaji wa uhakika katika hali halisi ya kila siku, ukiachilia mbali sheria ya makosa ya kujamiiana ambayo katika tisini na elfu mbili inatoa mwongozo wa mwenendo na adhabu kwa makosa yahusuyo ngono na ukiukaji wa haki za kimaumbile.
Hata hivyo, kama wengi walivyokwishasema, sheria ya makosa ya kujamiiana haikutengua wala kubatilisha sheria ya ndoa ya 1971 na kwa sababu hiyo sio mbadala wake. Moja ya madhara yake ni kuwepo kwa vifungu na vipengele kadhaa vinavyopingana na sheria ya ndoa ikiwa ni pamoja na umri wa anaetakiwa kuitwa mtoto kisheria.
Hii inaathari sana kwa utakelezaji wa sheria hizo pamoja na nyingine zinazohusu masuala ya uzazi na haki za vijana na wanawake kwa kuwa kila mkinzano ni kipenyo kinachoweza kuruhusu upindishaji wa sheria na hivyo kunyima haki mabalimbaliambazo makundi yangeweza kupata kisheria.
Juhudi zimekwisha kufanywa na serikali kujaribu kufanya mapitio ya sheria za ndoa nchini tangu mwishoni mwa miaka ya tisini zinaeleweka na kuheshimiwa nasi kama raia.
Hata hivyo changamoto kubwa hivi sasa kwa watanzania wa kawaida na jumuia za kiraia ni kuanzishwa kwa tume ya kurekebisha sheria ya mwaka1983,moja ya sheria zilizofikiriwa kama zinahitaji marekebisho makubwa au mabadiliko kabisa imekuwa ni pamoja na sheria hii ya ndoa ya 1971.
Chakushangaza na kusikitisha ni kuwa zaidi ya miaka ishirini sasa tangu kuanzishwa kwa tume hiyo, na miaka ipatayo kumi tangu kuanza kufikiria marekebisho ya sheria ya ndoa , hakuna kinachoonekana kama matokeo ya mchakato huo.
Aidha, miaka kumi baaada ya tume kurekebisha sheria kukabidhi ripoti yenye dondoo zenye haja na nia ya kubadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa waziri wa sheria na mambo ya katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna kikubwa kilichofanyika kama hatua ya wizara kutekeleza mapendekezo ya Tume ya kurekebisha sheria.
Mbaya zaidi ni ukimya uliotanda suala zima la haja ya marekebisho ya sheria hii kutoka wizarani, watoto na vijana wa nchi hii-wasichana kwa wavulana ambao ndio walio wengi kuliko makundi mengine yaliyobaki.
Kulikoni ukimya na usiri huu katika suala la hili? Kuna masuala kadhaa ya mkanganyiko katika sheria ya ndoa na sheria zingine zihisuzo masuala ya ndoa na yanayohusiana nayo.
Jambo la awali ni kutokuwa na makubaliano juu ya umri wa anayetakiwa kuwa mototo au kijana. Wakati katiba ya Jamhuri inatambua mtu wa miaka chini ya kumi na nane kama mototo na hivyo hawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za siasa, uchumi na jamii, umri wa kolewa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni miaka miaka kumi na tano kwa idhini ya wazazina hata kumi na nne kwa idhini ya mahakama.
Hapa pana tatizo kubwa na hata sio moja.Mtu anaeza akajiuliza ni vipi sheria kama hii iwepo iwepo hadi leo katika nchi kama Tanzania , nchi ijulikanayo na kusifiwa kama nchi ya kidemokrasia kote ulimwenguni .
Na pia kama ndoa ni mapatano au makubaliano kati ya watu wawili Mwanamke na Mwanamke – kwa ridhaa yao na utashi wao kamili,juu ya nini ulazima wa kuanza kuhitaji ridhaa ya wazazi katika kufungisha ndoa kati ya mwanaume aliye utu uzima na mototo wa kike wa miaka kumi na tano?
Tena , ni mapatano au makubaliano gani huru yanatakiwa kutafutiwa ridhaa ya mahakama kama inavyotakiwa mototo wa kike wa miaka kumi na nane anapolazimishwa kupatana na mwanaume wa umri wa mtu mzima?
Kwa maoni yangu huu ni ubaguzi na unyanyasaji mkubwa wa kijinsia ambao kwa miaka yote hii umeathiri vibaya haki na afya ya kiuzazi kwa watoto wa kike ikiwemo kusababisha vifo wakati watoto hao wa kike wanapojiribu kujifungua mtoto kabla ya maumbile muafaka kutimia.
Aidha, watoto wengi wa kike walioolewa katika umri wa miaka kumi na nne na wazee wa miaka arobaini mpaka hamsini wameishia kushindwa majukumu na kutelekezwa, wakiachwa wakiwa hawana msaada kijamii na kiuchumi kwa maisha yao kuvurugika kabla ya wakati.
Sambamba na hilo ni suala jingine lihusulo haki mbalimbali za watoto zinazokiukwa kwa kuozeshwa kabla ya umri wa mtu mzima . Ni hesabu ndogo sana kujua kuwa kama watoto anaanza shule katika umri wa miaka 7 hadi 11 kwa mujibu wa sheria ya Elimu ya mwaka 1978, basi atakuwa na umri wa kati ya mika kumi na nne mpaka kumi na nane anapomaliza elimu ya msingi, ambayo kwa sheria hii ni ya lazima kwa wote.
Kumwozesha mtoto katika umri chini ya miaka 18 si tu kumnyima mtoto huyo haki yake ya msingi ya kupata elimu bali pia ni uvunjaji wa sheria ya nchi ambao unastahili adhabu kali.
Aidha, sheria hii ya elimu inatoa adhabu kali kwa wanaozini na wanafunzi kwa kuwa wanahatarisha maendeleo ya wanafunzi kimasomo.
Hayamkini kuwa sheria hii imewekwa pembezoni na ndoa zinafungishwa katika umri wa miaka kumi na nne mpaka kumi na nane na kuitwa ndoa halali kwa mjibu wa sheria ya ndoa ya 1971.
Hapo haijazungumzwa haki ya mtoto aliyeolewa kupata elimu ya sekondari na hata elimu ya juu ambayo ni muhimu katika kufuta umasikini wa jamii yoyote duniani.
Katika kipindi hiki ambapo wanafunzi wanafurahia kumaliza elimu ya msingi na kujiandaa na hatua nyingine ya kuendelea mbele kimasomo wapo baadhi ya wazazi aidha kwa kutokujua au kukingwa na ubovu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 wanafurahia kupokea mahari kwa kuwaoza mabint zao wangali wadogo na hata matokeo ya hatma ya elimu yao yakiwa hayajajulikana.
Imefika wakati sasa mchakato wa kuelekea kuandika katiba mpya uainishe mambo muhimu yaliyosahaulika kama hili. Ipo haja ya jitihada za ziada kufanyika ili kuondokaza na tatizo hili linalozidi kuiweka nchi yetu katika wimbi la umaskini kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi katika hali duni na ya kimaskini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment