08 October 2012

Madenge aanza kazi kwa mbwembwe CCM



Na Anneth Kagenda

MWENYEKITI mpya wa Wilaya ya Kinondoni kupitia (CCM) Bw. Salim Madenge ameanza kazi kwa mbwembwe huku akitoa maagizo lukuki ya utendaji na kumtaka Katibu wa Wilaya hiyo Bw.Edwin Milinga na makatibu wengine kushuka chini na kwenda kuangalia utendaji kazi na uhai wa chama hicho.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa Ofisi Dar es Salaam jana Bw.Madenge alimwambia katibu huyo kuwa atabaki na kabila lake na kila kitu chake, lakini suala la mustakabali wa siasa atatakiwa amsikilize yeye kutokana na kwamba mchakato uliopo hivi sasa ni kuhakikisha wanaokoa Kata 32 na majimbo matatu yaliyoenda upinzani.

"Haya maagizo kila mtu kwa nafasi yake lazima ayatekeleze...viongozi wote wa Kata shukeni kwenye matawi mkaondoe makundi, muangalie uhai wa chama na mzungumze na wanachama kuanzia Oktoba 8

"Na pia muwe na taarifa zote, mwenezi fanya utaratibu wa kukutana na viongozi wa Kata na muandae wanachama na kuangalia nyendo za chama na mjibu mapigo ya wapinzania,"alisema Bw. Madenge.

Pia alimtaka mchumi kukutana na wachumi wenzake ili kuangalia jinsi ya kuboresha miradi ili iweze kuboreshwa, ambapo alimwambia Katibu Milinga kama kuna mtu anadai madeni yake basi ayawasilishe mezani kwake huku akisema kuwa kwa yeyote anayedai chochote katika wilaya hiyo atalipwa stahiki yake.

"Tumechaguliwa ili kuhakikisha chama kinasonga mbele hivyo basi mjue kwamba majungu kwangu mwiko na atakayeniletea majungu nitamuumbua, kwani kuna watu wanalipa nauli zao na kupanda daladala kwa ajili ya kuleta majungu wilayani hawa waache mara moja kwani mi niko kikazi zaidi na Ibara ya 5 (5) ya mwaka 2005 inazungumzia kushika dola na si vinginevyo ni lazima hili litimie," alisema Mwenyekiti huyo.

Naye Mwenyekiti mpya wa Wilaya ya Temeke, Bw. Yahya Sikunjema alisema awali vichwa vilivyokuwepo katika wilaya hizo mbili vilikuwa vimechoka hivyo mambo mengine kushindwa kuendelea huku akitolea mfano wa mabehewa ya treni yanayoshindwa kufika hata Morogoro.

"Chama hiki lazima kifike mahali kiendeshwe na vichwa vilivyochangamka kwani waliona hivi vichwa vilivyopo hata mabehewa yake hayawezi kufika Morogoro wala Kigoma na sasa hivi walivyoweka mabehewa yake yatafika huko na hivi vingine vikae pembeni ili chama kisonge mbele," alisema.

Naye Katibu wa Wilaya hiyo Bw. Milinga alisema hivi sasa chama hicho kimejikita katika mambo manne ikiwa ni pamoja na kuwa na mshikamano, umoja na nguvu kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa, kurudisha Kata walizoazima kwa upinzani, ambapo alisema kuwa programu za kuwamaliza wapinzani zitaandaliwa na ili kufikia 2014/2015 CCM iweze kuongoza kwa asilimia zote.



No comments:

Post a Comment