01 October 2012

Ludewa watakiwa kujiandaa kupokea wawekezaji mgodini

Na Nickson Mahundi,
Ludewa

WANANCHI wilayani Ludewa wametakiwa kujiandaa na ujio wa wageni zaidi ya 600,00 ambao watakuja katika machimbo ya migodi mikubwa ya Mchuchuma na Liganga iliyoko wilayani humo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Madaha jana katika ufunguzi wa kikao cha kamati ya Ushauri(DCC)cha wilaya ya Ludewa kutokana na mashirika na wageni mbalimbali kuanza kuingia katika wilaya hiyo iliyoko jirani na nchi ya Malawi.

Bw.Madaha alisema shirika la maendeleo la Taifa(NDC) limeandaa mpango wa uwezeshaji shirikishi kwa wananchi wa wilaya hiyo ili kuwaandaa
wananchi hao katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na kuwawezesha kutoka
katika wimbi la umaskini.

Alisema shirika la maendeleo la Taifa limemuandaa mtaalamu kutoka nchini Afrika Kusini kuja katika wilaya ya Ludewa ili kuandaa mpango mkakati wa maendeleo na elimu shirikishi kwa wananchi ili kupunguza migogoro kati ya wawekezaji na wananchi na kuwapa fursa ya kujitambua.

“NDC imempata mtaalamu kutoka nchi ya Afrika kusini kuja hapa kuuandaa mpango wa maendeleo hivyo nawaomba wananchi kujiandaa na ujio wa
wageni kwani kutakuwa na changamoto kubwa kutoka kwao,"alisema.

Aliwataka wananchi kujiandaa na zoezi la utoaji maoni katika katiba mpya, kwani zoezi hilo katika wilaya ya Ludewa linatarajia kufanyia kazi kuanzia Oktoba 8 hadi 13 mwaka huu katika maeneo mbalimbali.

Bw.Madaha alisema katika zoezi la maoni ya katiba mpya  ni vema wananchi wakatoa maoni kwa kutumia akili yao na si kwa utashi wa mtu mwingine, chama chochote cha siasa au Dini kwa katiba ni muhimu kwa kila mtanzania.

Hata hivyo Bw.Madaha aliwapongeza wananchi kwa kushiriki vema katika zoezi la Sensa ya watu na makazi kutokana na zoezi hilo kufanyika vizuri katika wilaya ya Ludewa bila matatizo yoyote tofafauti na maeneo mengine.


No comments:

Post a Comment