08 October 2012
Bodi NBC yamrudisha Mafuru
Na Willbroad Mathias
BODI ya Wakurugenzi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), imetangaza kumrejesha kazini Mkurugenzi Mwendeshaji Bw. Lawrence Mafuru, baada ya kukamilika uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ndani ya benki hiyo.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana katika vyombo vya habari na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt. Mussa Juma Assad, alisema Bw. Mafuru atarejea kazini haraka baada ya kukamilika uchunguzi huo.
“Ulikuwa mchakato muhimu kwa wadau wote wakiwemo wateja, wafanyakazi, wanahisa na umma kwa ujumla, uchunguzi wa kina ulifanyika ili kuhakikisha uongozi wetu unaendesha benki hii kwa mujibu wa taratibu za uongozi bora,” alisema Bw. Asaad.
Alisema Julai 19 mwaka huu, bodi hiyo ilimuomba Bw. Mafuru, akakubali kwenda likizo ili kuruhusu uchunguzi wa makosa yanayodaiwa kufanyika ndani ya benki hiyo.
Aliongeza kuwa, bodi hili ilipokea tuhuma za ubadhirifu dhidi ya menejimenti ya benki hiyo hali ambayo ilisababisha kufanyika uchunguzi wa kina ili kudumisha maadili ya utawala bora.
Kwa upande wake, Bw. Mafuru, ambaye tayari amejerea kazini baada ya miezi miwili ya likizo kupisha uchunguzi huo alisema ni furaha kubwa kwake kuona uchunguzi huo umekamilika na ukweli kujulikana.
Alisema licha ya kuwa kipindi cha likizo kilikuwa kigumu kwake, hana kinyongo chochote kwani mchakato huo ulikuwa muhimu katika taasisi yao ambayo imekuwa ikisifika kwa utawala bora.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment