08 October 2012

Azam yatamba kuendelea kuwa juu


Na Speciroza Joseph

BAADA ya kuifikia Simba kilele mwa Ligi Kuu Bara, Kocha wa Azam FC, Boris Bunjak 'Boca', amesema atahakikisha timu yake inaendelea kukaa katika nafasi za juu hadi kumalizika kwa msimu huu wa ligi.

Kocha wa huyo alitoa kauli hiyo muda mchache baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi hiyo kati ya Azam na African Lyon, mchezo uliopigwa juzi Uwanja wa Azam Complex na wenyeji kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na John Bocco 'Adebayor'.

Matokeo hayo yaliiongezea pointi Azam FC na kufukisha pointi 13 sawa na Simba (kabla ya mechi ya jana) wakitofautiana kwa idadi ya mabao.

Kocha huyo alisema timu yake imeonyesha uwezo katika michezo yote mitano waliyocheza pasipo kupoteza mchezo wowote, hivyo anaamini wakiongeza juhudi zaidi nafasi yao katika ligi kuu itakuwa juu muda wote.

"Tunatarajia kushinda ili tusiondoke katika nafasi za juu, kufanya hivyo kutakuwa na manufaa kwa timu na kumaliza ligi tukiwa mabingwa ama washindi wa pili" alisema kocha huyo.

Akizungumzia michezo mitano aliyocheza, kocha Boris alisema mechi zote zilikuwa ngumu, hajakutana na mechi rahisi hivyo anaiona ligi hiyoinahitaji umakini na jitihada zaidi ili kuweza kushinda.

Akielezea mchezo wao dhidi ya Lyon, kocha huyo alisema ulikuwa mchezo moja kati ya mechi nzuri alizokutana nazo kwa kuwa timu hiyo imeweza kuzuia mashambulizi ya wachezaji lakini walitumia kosa lao moja kupata ushindi.

Alisema kipindi cha kwanza wachezaji wake walicheza vizuri zaidi na kipindi cha pili baada ya mabadiliko timu ikawa katika hali nzuri ya kulinda ushindi huo ambao uliwapa pointi tatu muhimu.

Azam mechi  inayofuata itacheza na Polisi Moro kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kabla ya kwenda mkoani Mbeya kucheza na Tanzania Prisons.

No comments:

Post a Comment