25 September 2012

Yanga, Simba zaingiza milioni mil. 143.7/-


Na Zahoro Mlanzi

MECHI za mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba dhidi Ruvu Shooting na ile ya Yanga dhidi ya JKT Ruvu, zimeingiza sh. 143,705,000 kutokana na jumla ya watazamaji 65,458 kwa mechi zote walioingia uwanjani.


Michezo hiyo ilipigwa mwishoni mwa wiki, ambapo Yanga ilianza Jumamosi dhidi ya JKT na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 na Simba ikacheza Jumapili na kushinda mabao 2-1.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kwamba mechi ya Yanga iliingiza sh. 88,251,000 na ile ya Simba mapato yalikuwa sh. 55,454,000.

"Katika mechi ya Yanga kila timu ilipata sh. 19,846,194.92 ambapo mashabiki 15,770 walishuhudia mechi hiyo huku ile ya Simba kila timu ilipata sh.11,350,774.58 kutokana na mashabiki 9,688," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati huohuo, Wambura alisema wameridhishwa na kuongezeka kwa mapato kwenye Uwanja wa Azam Complex, kutokana na mapato ya sh. milioni 2.5 yaliyopatikana katika mechi dhidi ya Azam FC na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Aliongeza pia mechi ya African Lyon na Tanzania Prisons iliyochezwa juzi kwenye uwanja huo iliingiza sh. sh. 245,000 huku kila timu ikipata sh. 32,286 katika mechi hiyo Prisons ilishinda kwa mabao 2-1.

Akizungumzia zaidi suala la mapato kwenye uwanja huo, Wambura alisema kama timu ikihitaji ipate mgawo mkubwa haina budi kuitangaza timu yao na kucheza soka la uhakika, ambapo wana imani mashabiki wao watajitokeza kwa wingi.


No comments:

Post a Comment