25 September 2012

Milovan: Siihofii Yanga hata kidogo *Adai kila mechi kwake ni fainali



Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema hawezi kuiwazia mechi moja tu dhidi ya Yanga ya Oktoba 3, mwaka huu kwani kila mechi anaichukulia kwa uzito mkubwa, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom.


Akizungumza Dar es Salaam juzi, mara baada ya mechi yao na Ruvu Shooting ambayo walishinda mabao 2-1, Milovan alisema bado kikosi chake kina kumbukumbu nzuri ya kuwafunga watani zao hao mabao 5-0, hivyo hawana presha na mechi hiyo kama itakavyokuwa kwa mahasimu wao ambao watataka kulipa kisasi.

"Mimi siangalii mechi moja dhidi ya Yanga, naangalia kila mechi ambayo tutacheza ili tuweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa, kila mechi naichukulia kama ni mechi ya fainali," alisema Milovan

Akizungumzia mechi ya Ruvu Shooting, Milovan alisema pamoja na kuwepo na upungufu katika kikosi chake, lakini wachezaji wake walitumia juhudi binafsi na hivyo kuwafanya waondoke na pointi tatu.

"Lengo langu ni kuendelea kushinda kila mechi kwani hii itatusaidia mno pindi tutakapoanza kucheza ugenini ni muhimu kushinda mechi nyingi za nyumbani na nimeshazungumza na wachezaji wangu kwamba sasa hivi ni vita, kwani kila timu inataka pointi tatu," alisema.

Alisema bado ataendelea kukirekebisha kikosi chake kwani amegundua upungufu mkubwa, hivyo atafanya hivyo kabla ya kuvaana na Prisons ya Mbeya Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Milovan alisema watakuwa na muda wa kutosha kabla ya kuvaana na Prisons hivyo hana wasiwasi na hilo, huku wakiwataka wachezaji wake waongeze bidii zaidi ili wahakikishe wanazoa pointi katika mchezo huo unaotabiriwa kuwa na upinzani mkali.

Akiwazungumzia mabeki wake Komalmbil Keita na Patrick Ochieng, Milovan alisema anazidi kuwanoa vizuri mazoezini ili waweze kuzoenana na wenzano.

No comments:

Post a Comment