05 September 2012
Yanga sasa yakamilika idara zote *Nurdin arudi kundini
Na Zahoro Mlanzi
KIUNGO wa mabingwa wa Kombe la Kagame Yanga, Nurdin Bakari jana ameanza mazoezi na wenzake yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Loyola, Dar es Salaam baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Mbali na kiungo huyo, Athuman idd 'Chuji' ambaye pia alikuwa mgonjwa ameanza mazoezi lakini kipa, Said Mohamed atakosa mazoezi kwa wiki chache zijazo baada ya kuwa mgonjwa.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema Nurdin alianza mazoezi rasmi jana na wenzake baada ya kukosekana uwanjani kwa zaidi ya miezi mitatu akisumbuliwa na kifundo cha mguu.
"Tunashukuru timu inazidi kuimarika kwani Nurdin, ameanza mazoezi pamoja na Chuji ambaye alikuwa mgonjwa sasa hivi sehemu ya kiungo inazidi kuwa na ushindani, hivyo ina maana sasa kila mmoja atacheza kwa kujituma," alisema Sendeu.
Alisema wakati viungo hao wakiongeza nguvu kipa, Mohamed atakosekana kutokana na kusumbuliwa na malaria, hivyo atakapopata nafuu hakuna shaka atajiunga na wenzake.
Akijibu swali kuhusu mechi dhidi ya SOFAPAKA, iliyotangazwa kuchezwa mwishoni mwa wiki, alisema: "Hatuna taarifa na mechi hiyo na tunashangaa imetangazwa bila ya sisi kuhusishwa.
Aliongeza kwamba kwa sasa hawana programu za mechi za kirafiki kutokana na kocha, Tom Saintfeit kutoomba mechi yoyote lakini itakapotokea hivyo watatoa taarifa.
Wakati huohuo, timu hiyo kesho inatarajia kutembelea Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), baada ya wiki iliyopita kuahirishwa ambapo watakwenda kujionea jinsi kampuni hiyo inavyotengeneza bia ya Kilimanjaro Lager, ambayo ndiyo wadhamini wa timu hiyo.
Akizuzungumzia suala hilo, Sendeu alisema mbali na hilo pia watatapata fursa ya kula chakula cha mchana na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, ikiwa ni sehemu ya kudumisha uhusiano wao mzuri na kampuni hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment