05 September 2012
Yanga yaikwepa Sofapaka, sasa kucheza na Simba SC
Na Elizabeth Mayemba
BAADA ya Yanga kuchomoa kucheza na Sofapaka ya Kenya, timu hiyo inatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Simba itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
.
Awali Sofapaka walitarajia kucheza na Yanga leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam lakini hadi jana mchana timu hiyo ilikuwa haijathibitisha kucheza mechi hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mratibu wa mechi hiyo, George Wakuganda alisema wameachana na mechi ya leo, ambayo Yanga ilikuwa icheze na Sofapaka na badala yake timu hiyo kutoka Kenya itacheza na Simba keshokutwa.
"Yanga walikuwa wacheze kesho (leo) na Sofapaka, lakini hadi hivi tunavyoongea hawajajibu kitu, hivyo tumeamua kuifuta mechi hiyo na badala yake Sofapaka watacheza na Simba keshokutwa na wanatarajiwa kutua Jumanne," alisema Wakuganda.
Alisema wameamua kuileta timu hiyo kutoka Kenya kutokana na uwezo mkubwa wa timu hiyo, hivyo wana imani itakuwa ni kipimo tosha kwa Simba wanaojiandaa na mechi yao ya Septemba 11 ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC.
Kwa upande wake Simba, Kocha Mkuu wa timu hiyo Milovan Cirkovic alisema mechi hiyo itamsaidia kuangalia kikosi chake na itakuwa ni mwendelezo wa mechi zao za kirafiki za kimataifa.
Timu hiyo ilianza kucheza na Mathare United ya Kenya na kushinda mabao 2-1 na mwishoni mwa wiki, ilicheza na timu nyingine kutoka Kenya ya Soni Sugar.
"Ni kipimo kizuri kwa wachezaji wangu na ninajua ni wapi natakiwa kufanyia marekebisho kwani tunakabiliwa na mechi yetu ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, pamoja na Ligi Kuu itakayoanza kutimua vumbi Septemba 15 mwaka huu," alisema Milovan.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment