28 September 2012

Wiki ya Soka Tanzania kuanza kwa Azam, JKT leo



Na Elizabeth Mayemba

WIKI ya Soka Tanzania (Super Weekend), inaanza leo wakati timu za Azam FC na JKT Ruvu zitakapocheza mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuazia saa moja usiku.


Mechi hiyo na nyingine nne zinatarajiwa kurushwa moja kwa moja na Super Sport.

Mbali ya Azam na JKT Ruvu mechi itakayofuatia kurushwa na Super Sport ni ile ya kesho kati ya Simba na Prisons  kuanzia saa 11 jioni na keshokutwa Yanga na African Lyon nayo ni saa 11 jioni zote kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam, Jumatatu ni zamu ya Ruvu Shooting na Mtibwa ambao mechi yao itachezwa Uwanja wa Azam, Chamazi Dar es Salaam kuanzia saa 10:30 jioni.

Mechi ya mwisho kurushwa na Super Sport ni ile ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kati ya miamba miwili ya soka nchini Simba na Yanga, ambapo mechi yao itachezwa Jumatano ijayo, mechi hiyo pia itaanza saa 1:30 jioni.

Akizungumzia mechi ya leo, Kocha Msaidizi wa Azam FC Kally Ongala alisema wachezaji wake wapo fiti kwa ajili ya mechi ya leo, na wanatarajia kuondoka na ushindi ili waweze kukaa kileleni kwani wakishinda watakuwa wamefikisha pointi 10.

"Sisi tumejiandaa kwa kila mechi na lengo letu ni kuondoka na ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi, ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya mwaka jana kuishia nafasi ya pili," alisema Ongala.

Alisema timu zote zinazoshiriki ligi kuu zimepania hivyo hawatakiwi kuzembea hata mara moja, kwani kosa moja linaweza kuwagharimu sana hivyo watakuwa makini sana kwa hilo.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanaongoza kwa pointi 9 wakiwa hawajafungwa mechi hata moja wakifuatiwa na Coastal Union wenye pointi nane wakiwa wameizidi simba mchezo mmoja, Azam FC wao wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi saba, huku JKT ambao watacheza nao leo wakiwa nafasi ya tatu kutoka mwisho wakiwa na pointi tatu.

No comments:

Post a Comment