28 September 2012

Milovan asema Yanga kipigo palepale *Wenyewe wakutana kupanga mikakati ya kuwamaliza



Na Elizabeth Mayemba

MABINGWA wa Tanzania Bara Simba  wapo katika mazoezi mazito visiwani Zanzibar, ambako walikwenda Jumanne iliyopita kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Oktoba 3, mwaka huu dhidi ya Yanga wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Timu hiyo inatarajia kurudi  kesho Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wao na Prisons ya Mbeya na kisha kurudi tena visiwani humo.Simba wamekuwa wakifanya mazoezi yake katika Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe na kambi wameweka Chukwani.

Akizungumza kwa simu kutoka Zanzibar Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic alisema, timu yake ipo vizuri na wachezaji wanaendelea na mazoezi ili kuhakikisha hawapotezi mechi zao zote za nyumbani, ikiwemo ile ya Yanga.

Alisema ole wao Yanga wanaojidanganya kuwa watawafunga, kwani wachezaji wake wamemhakikishia kutofanya makosa katika mchezo huo ili kuendeleza raha kwa mashabiki wao.

"Vijana wangu wapo vizuri na wanaendelea na mazoezi kama kawaida lengo ni kutaka tufanye vizuri katika mechi zetu zote za nyumbani, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa, Yanga wasijidanganye hata kidogo," alisema Milovan

Hata hivyo, katika michezo miwili ijayo Simba itamkosa mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi ambaye amefungiwa na Kamati ya Ligi kucheza mechi tatu sambamba kumtoza faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.

Tayari Okwi amekosa mechi moja  dhidi ya Ruvu Shooting hivyo atakosa tena ya kesho dhidi ya Prisons na ile ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru.

Wakati Simba, wakiwa Zanzibar Yanga wao wapo Changanyikeni, ambapo Kocha Msaidizi wa timu hiyo Freddy Felix Minziro, amesema kuwa hana hofu na mechi hiyo ya Jumatano ijayo kwa kuwa jeshi lake limekamilika, hivyo Simba walie tu.

Kocha huyo alisema hana presha na mechi hiyo kwa kuwa wapinzani wao anawafahamu vizuri na wanachotaka wao ni kulipa kisasi kwani mashabiki wao wanataka kufuta machungu siku hiyo.

"Watani zetu Simba hizo ni kelele za chura tu hazimzuii tembo kunywa maji, acha watambe, lakini mwisho wao ni Jumatano ijayo," alisema.

Wakati huo huo matawi ya Yanga jana yalikutana  katika kikao maalum kujadili namna ya kuifunga Simba, huku wakionekana kukasirishwa na matokeo yaliyopita pindi walipokutana na watani zao hao na kufungwa mabao 5-0.

Ajenda kuu, ilikuwa ni jinsi kuifunga Simba na watu wakagawana majukumu kwa makubaliano ya kuanza utekelezaji mara moja.

No comments:

Post a Comment