18 September 2012

Watatu wafariki katika matukio tofauti Dar


Na Neema Kalaliche

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti jijini Dar es Salaam, likiwemo la mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Bi. Catherine John (48), kujinyonga kwa kanga.


Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tukio hilo limetokea jana asubuhi makutano ya Kawawa ambapo marehemu John alikutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga.

“Inaaminika saababu iliyomfanya ajinyonge ni kukata tamaa ya maisha kwani alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa UKIMWI pamoja na vidonda vya tumbo,” alisema.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na upelelezi unaendelea.

Katika tukio jingine, mkazi wa Mzambarauni Ukonga, Rashid Omary (17), amefariki dunia baada ya kugusa swichi ya umeme iliyokuwa wazi na kunaswa. 

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Komba, alisema marehemu alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Amana ambapo mwili wake umezikwa jana.

Wakati huo huo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, David Misime, alisema chumba kimoja cha baa inayofahamika kwa jina la Sikinde, iliyopo Temeke inayomilikiwa na Bi. Hadija Shabani, kimeteketea kwa moto na kuunguza vifaa mbalimbali.

Alisema chanzo cha moto huo ni mshumaa lakini moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto cha Jiji la Dar es Salaam ambapo  mali zilizoungua thamani yake haijafahamika na uchunguzi unaendelea.

No comments:

Post a Comment