19 September 2012

Wanasheria: Tuhuma za majaji sasa zichunguzwe



Na Agnes Mwaijega

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika Law Society (TLS),  kimemtaka Rais Jakaya Kikwete na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, waunde tume ambayo itachunguza tuhuma zilizotolewa kwa majaji katika Kikao cha Bunge la Bajeti, mjini Dodoma ili wananchi waendelee kuwa na imani na muhimili huo.

Tamko hilo limetokana na kauli iliyotolewa bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, Bw.Tindu Lissu (CHADEMA), kuwa baadhi ya majaji hawana uwezo na sifa za kushika wadhifa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa TLS, Bw. Francis Stolla, alisema madai hayo ni mazito hivyo yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi ili jamii iendelee kuwa na imani na watendaji wa mahakama.

Alisema tangu Bw. Lissu atoe tuhuma hizo, hawajaona hatua zozote ambazo zinachukuliwa sambamba na kufuatilia ukweli wa madai ya kuwepo majaji wasio na sifa kimaadili na kitaaluma.

Aliongeza kuwa, tuhuma hizo zimejenga taswira mbaya kwa wananchi na kufanya imani yao kwa mahakama kupungua.

“TLS haijawahi kufanya utafiti ili kupata ukweli wa madai haya lakini kama itabainika zina ukweli hasa kwa majaji waliotajwa, mamlaka husika ihakikishe inautangazia umma,” alisema.

Akizungumzia mauji yaliyotokea nchini na polisi wakionekana kuwa wahusika wakuu, Bw. Stolla, alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu za ziada ni kimyume cha sheria.

1 comment:

  1. SIKILIZENI NYIE TLS NCHI HII IMEOZA KWENYE SHERIA,MAWAKILI NDIO WABAYA ZAIDI WAKISHIRIKIANA NA HAO MAJAJI NA MAKARANI WA MAHAKAMA NA KUVURUGA MFUMO WOTE WA SHERIA NCHINI. KINACHOHITAJIKA SASA KUFUMULIWA KOTE KUANZIA MAJAJI, MAKARANI NA MAWAKILI. TUNAHITAJI TUME HURU YA UTUMISHI WA MAHAKAMA AMBAO MAJAJI NA MWANASHERIA MKUU NA JAJI MKUU HAWATAKUWEPO MAANA HAWA UKIWAPELEKEA MALALAMIKO HAWASHUGHULIKI NI KWA NJIA GANI TENA HAWAHAWA WAWEPO KWENYE TUME KUJADILI MALALAMIKO YAKO. KUNA JAMBO LIMEJIFICHA TLS

    ReplyDelete