19 September 2012

Ajifungua mtoto wa ajabu *Kichwa kinafanana na ndama wa ng'ombe


Na Esther Macha, Chunya

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Kijiji cha Maganga, Kata ya Mbuyuni, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, Bi. Shija Paulo (35), amejifungua mtoto wa kiume ambaye kichwa chake kinafanana na ndama wa ng'ombe.


Tukio hilo la ajabu limetokea Septemba 16 mwaka huu, saa 11 alfajiri, baada ya Bi. Paulo kushikwa na uchungu hivyo mumewe Bw. Mwigulu Yangula, aliamua kumkimbiza kwa mkunga wa jadi aliyekuwa jirani na nyumba yao.

Mkunga huyo Bi. Sikanyika Fredick, alimsaidia Bi. Paulo ambaye alijifungua salama ambapo kichwa cha mtoto huyo, kilifanana na mtoto wa ng'ombe (ndama), mwenye dalili ya kuota mapembe na manyoya meusi kuanzia kichwani hadi kifuani.

Kuanzia kifuani, mtoto huyo alikuwa na umbile la binadamu ambapo kiumbe hicho kilidumu kwa saa tatu na kufariki dunia kutokana na sababu ambazo hazikujulikana mara moja.

Mfanyakazi wa Kituo cha Afya, kilichopo Kitongoji cha Magaga Bw. Josephat Alisen, alisema hajawahi kukutana na tukio hilo tangu aanze taaluma ya utabibu.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Michael Sanziwa, hakuwepo wakati tukio hilo linatokea lakini aliagiza kiumbe hicho kichukuliwe na mzazi wake na kwenda kumzika.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamelihusisha tukio hilo na imani za kishirikina ambapo viumbe vya aina hiyo, mara nyingi haviishi muda mrefu lakini hali ya mama aliyejifungua inaendelea vizuri.


No comments:

Post a Comment