25 September 2012

'Wamiliki sekta ya miti, viwanda ibueni matatizo yanayowakabili'


Na Stella Aron

WAMILIKI wa mashamba ya miti na viwanda vya misitu Tanzania Bara na Zanzibar, wametakiwa kuibua matatizo waliyonayo kwenye sekta hizo ili yaweze kujadiliwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 24 mwaka huu.


Rais wa Shirikisho la Viwanda Vya Misitu nchini (SHIVIMITA), Bw. Ben Sulus, aliyasema hayo Dar es Salaam juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema naadalizi ya mkutano huo ambao utafanyika mkoani Morogoro na kushirikisha viongozi wa Wizara ya Malisili na Utalii na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), yanaendelea vizuri

“Mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, wadau katika sekta hizi wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ushirikishwaji serikalini na kukosekana kwa mpango mpango mkakati au dira ya maendeleo katika misitu.

“Tunawashauri wadau wote katika sekta hizi, washiriki mkutano huu ambao utajadili changamoto nyingi, namna ya kuzitatua na kuweka mpango mkakati na kuinua uchumi,” alisema.

Bw. Sulus alisema malighafi zilizopo ni chache ukilinganisha na mahitaji makubwa yaliyopo nchini hivyo kuleta usumbufu kwa wadau.

Aliongeza kuwa sekta hiyo inahitaji maboresho na kuwaomba wadau washirikiane na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Balozi Kagasheki ili kuendeleza sekta ya misitu na viwanda.

No comments:

Post a Comment