25 September 2012

CCM yamtimua Mwenyekiti wa kijiji



Na Yusuph Mussa, Korogwe

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Kijiji cha Goha, Kata ya Mazinde Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, kimemvua madaraka Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho Bw. Athuman Mangare kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya rushwa hasa uuzwaji wa ardhi.


Uamuzi huo umefikiwa juzi kwenye Mkutano Mkuu uliofanyika katika Shule ya Msingi Goha ambapo Bw. Mangare alipigiwa kura 80 za kutokuwa na imani nae wakati kura 18 zilitaka aendelee kubaki madarakani.

Akizungumza katika mkutano huo kabla mchakato wa kupiga kura haujaanza, Mwenyekiti wa CCM Tawi la Goha. Bw. Rashid Mdoe, alisema wamechoka kuwa na viongozi wanaokipata matope chama hicho kutokana na tuhuma za ufisadi.

Bw. Mdoe alitaja tuhuma za Bw. Mangare kuwa alishirikiana na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Bw. Thomas Richard, kumpa mwekezaji hekta 20 za kijiji kwa ajili ya kilimo cha mkonge bila kushirikisha wananchi.

“Nilimuagiza Bw. Richard amwambie Bw. Mangare kuwa eneo hilo la wananchi hivyo lisipewe mtu bila Mkutano Mkuu wa kijiji au halmashauri ya kijiji na wote niliwaita katika mkutano wa leo (juzi), ili wajieleze lakini Mtendaji alikuja kuchungulia na kuondoka.

“Bw. Mangare amekataa kuja maana yake amenipuuza mimi kama bosi wake, ameenda sehemu nyingine ambayo anaamini atatetewa ili aweze kurudi madarakani,” alisema Bw. Mdoe.

Wakichangia katika mkutano huo ambao pia ulishirikisha baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, Bw. Amir Zubeir, alisema vinara wa kuuza viwanja vya wananchi pamoja na mashamba ni wanne akiwemo Bw. Mangare na Bw. Richard, lakini risiti za uuzwaji huo hazionekani.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Bw. Mangare, alisema yeye bado ni Mwenyekiti na wanachofanya viongozi hao wa CCM ni mchezo wa kuigiza.

“Kuna ngazi za kufuata ili waweze kuniondoa madarakani, suala hili lilipaswa kupelekwa Kamati ya Siasa na baadae Halmashauri Kuu ya Kijiji, mimi sihusiki kumuuzia ardhi mwekezaji bali ameomba kupewa eneo husika,” alisema.

Naye Bw. Richard ambaye alikingiwa kifua na Bw. Mdoe asiondolewe madarakani, alisema viongozi wa CCM kijijini hapo wanampiga vita Bw. Mangare na kukanusha taarifa za wao kula fedha za viwanja, mashamba na kusisitiza mkutano ambao utaonesha maapato na matumizi utafanyika hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment