17 September 2012

Wakulima waruhusiwe kuuza mazao nje kuongeza pato la Taifa


Na Rose Itono

SERA ya kilimo ya mwaka 1997, inasisitiza kuwa endapo kilimo kitapewa kipaumbele zaidi, kitasaidia kuondokana na tatizo la njaa nchini, ikiwa ni pamoja na kuinua uchumi kutokana na kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi na hatimaye kujipatia fedha za kigeni.

Ilitungwa ili kuwezesha kuwepo akiba ya kutosha ya chakula na kubadilisha maisha ya wananchi waishio vijijini waongeze uzalishaji.

Asilimia kubwa ya maisha ya Watanzania hutegemea kilimo, kwa kutambua hivyo Mwalimu Julius Nyerere aliita ‘Kilimo Uti wa Mgongo.’

Pamoja na kauli hiyo, bado kuna kauli mbalimbali zilizoasisiwa na Mwalimu Nyerere pia viongozi wengine wa kitaifa kama ‘Kilimo cha Kufa na Kupona,’ ‘Kilimo cha Kijani’ ikiwa ni njia ya kuwatia moyo wakulima pamoja na kuongeza ufanisi wake kwa kutambua kwamba, kuyumba kwa kilimo ndio kuyumba kwa uchumi wa taifa.

Kwa kufanya hivyo, serikali kila mwaka hufanya juhudi kuhakikisha kuwa, wakulima nchini wanaboreshewa mazingira ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa, wanapata mavuno yanyoweza kuwanufaisha pamoja na kuongeza pato la Taifa
   
Kilimo ni sekta muhimu kwa maisha na uchumi wa wakazi wengi nchini kutokana na ukweli kuwa asilimia 80 ya watanzania wanakigemea kujipatia kipato.

Kutokana na hilo kuna kila sababu ya wakulima kutengenezewa mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kutafutiwa masoko ndani na nje ya nchi ili wazalishe kwa wingi.

Mazao makuu yanayolimwa nchini ni pamoja na mihogo, viazi vitamu, mpunga, mahindi, migomba na kunde. Mazao ya biashara ni korosho, minazi, mboga, matunda, maua na viungo.

Pamoja na maeneo makubwa ya mjini kutumika kama sehemu ya kuishi bado Kilimo cha (Mboga na matunda) huchangia kuimarisha lishe bora, mapato na uboreshaji mazingira.

Kutokana na hali hiyo upo umuhimu wa serikali kuimarisha mawasiliano na wakulima nchini ili waweze kuelewa taratibu wanazopaswa kuzifuata wanapotaka kuuza mazao yao nje ya nchi.

Bw. Ntimi Mwakinyuke mkulima kutoka wilaya ya Kilombero anasema kuwa, kumekuwa na upungufu wa taarifa za uuzaji wa mazao nje ya nchi kutoka serikalini pale kunapokuwa na zuio la kufanya hivyo hali inayopelekea kuwa njia panda.

"Utaratibu wa kuuza chakula nje ya nchi bado halijaeleweka  miongoni mwetu kiasi tunashindwa kusafarisha mazao yetu kwenda nje kwa wakati",anasema Bw.Mwakinyuke.

Anasema pamoja na kuwa na soko kubwa la chakula nje ya nchi bado wakulima hawapewi fursa ipasavyo.

“Mara ya mwisho nilipata oda ya mchele kupeleka nchi jirani lakini nikashindwa kufanya hivyo kutokana na utaratibu usioeleweka uliowekwa na serikali, ”anasema  

Anaongeza kuwa kuna haja ya kuimarishwa mawasiliano baina ya idara za serikali na wakulima ili kuwezesha kuelewa taratibu za uuzaji wa mazao nje.

Bi. Scolastika Thomas mkulima kutoka Igunga mkoani Tabora, aliishauri serikali kujenga utaratibu wa kutoa fidia kwa wakulima pindi inapoweka vizuizi vya kuuza nje mazao yao ili kurudisha gharama zao na kuwafanya kuendelea na kilimo kwa msimu unaofuata.

"Serikali ielewe ni kwa kiasi gani wakulima  wanaoumia kutokana na zuio la kuuza mazao yao nje na kuwafanya kudidimia kibiashara", anasema.

Anasema kuwa zuio la  mazao linawakosesha kipato wakulima kwani huwa hawaruhusiwi kuuza nje ya nchi.

“Inapotokea zuio la aina hii serikali haina budi kutufidia ili tuweze kuimarisha maisha yetu na kuendeleza kilimo,” anasema.

Anafafanua kuwa, wakulima wamekuwa wakizalisha mazao mengi lakini hawana soko la uhakika kutokana na ubovu wa miundo mbinu hivyo kwa kupata soko la nje kutawezesha kuongeza kipato.

Kwa upande wake Bw. Godfrey Bwana kutoka kampuni ya kuendeleza wakulima vijijini  yenye makao yake mkoani Dodoma anasema kuwa vikwazo vya kuuza mazao havisaidii katika kuongeza uzalishaji wala kupunguza umaskini.

Anapendekeza serikali kufanya utafiti wa kutosha hasa pindi inapotaka kuweka vikwazo vya mazao ya nafaka ili kuwezesha wakulima kunufaika na kilimo hicho.

Bw.Bwana anasema kuwa wakala wa chakula nchini (NFRA) inatakiwa kupata nafaka za kutosha kwa bei ya soko hasa kipindi cha mavuno.

“Serikali inatakiwa kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kuhifadhi nafaka, sera za uzalishaji na teknolojia pia kuhuwisha biashara ya Afrika mashariki,” anaongeza.

Mkurugenzi wa usalama wa chakula kutoka wizara ya Kilimo, chakula na ushirika Bw Karim Mtambo, anasema serikali inaweka zuio la mazao inapojiridhisha kuwa kuna upungufu wa chakula.

Anasema serikali nyingi duniani huchukua hatua hizo pindi inapoonekana kuwa usalama wa chakula ni mdogo, kwani unaweza kuleta mapinduzi ya utawala.

Hata hivyo anabainisha kuwa tayari serikali imekwisha ondoa amri ya zuio la kuuza nje mazao na sasa wakulima wanaruhusiwa kuuza.

“Kinachotakiwa ni kupata ruhusa kutoka kwetu kwa ajili ya utunzaji wa kumbukumbu na hatimaye kuuza mazao yake nje,” anafafanua.

Bw.Mtambo anabainisha kuwa mbali na kutoa zuio hilo, bado kuna baadhi ya mikoa inakabiliwa na uhaba wa chakula ikiwemo Shinyanga, Kilimanjaro, Dodoma, Arusha na  Mwanza.

Mdahalo huo uliokuwa ukijadili madhara yanayowapata wakulima kwa kuzuia kuuza mazao nje ulishirikisha wadau 70 na  kwamba ulikuwa na lengo la kujadili mbinu bora za kumuwezesha mkulima kufanya kazi zake bila vikwazo na kupeleka mapendekezo serikalini.





No comments:

Post a Comment