17 September 2012

Tushirikiane kupinga ukatili kwa wajane



Na Agnes Mwaijega

MOJA ya masuala ambayo yamekuwa yakipingwa vikali nchini ni vitendo vya kikatili na kibaguzi dhidi ya wanawake hasa wajane kwa sababu vinakwamisha ustawi wa maisha yao.

Hata hivyo, kadri siku zinavyodhidi kusonga mbele ndivyo vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka na kuonekana kwamba ni vya kawaida wakati waathirika wanaumia na kukosa haki zao za msingi.

Katika jamii zetu tunasikia na kushuhudia wajane wakiathirika na mila potofu za kupigwa, kurithiwa na hata wengine kuuawa kwa kuhisiwa kwamba ni wachawi ili mradi tu ndugu wa marehemu wapate mwanya wa kujitwalia mali za ndugu yao.

Wakati mwingine wamekuwa wakifukuzwa kwenye nyumba walizoachiwa na marehemu waume zao kwa kisingizio kwamba wao ndiyo wamesababisha vifo vyao.

Katika makabila mengine wajane wanarithiwa na mashemeji zao kutokana na mila na desturi mbovu ambazo hazina manufaa yoyote.
 
Hali hiyo imesababisha wajane hao kukosa mahali pa kukimbilia kwa sababu mila na desturi za sehemu wanazotoka ni kandamizi na zinawanyima haki.

Juhudi zao za kujikomboa zimekuwa zikikwama hata wanapokwenda mahakama kupitia asasi zisizo za kiserikali zinazotetea haki za binadamu kutokana na kuwepo kwa sheria kandamizi.

Mojawapo ya sheria kandamizi ambayo inasababisha wajane kuendelea kuteseka ni ile ya kimila ya 1963 kifungu cha 27 cha sheria ambacho kinatamka kuwa mjane hana fungu lake katika urithi ikiwa marehemu aliacha jamaa na ukoo wake na fungu  lake ni kutunzwa na watoto wake jinsi alivyowatunza.

Kutokana na kifungu hicho wajane wamekuwa wakinyang'anywa hata mali ambazo walichuma kwa kushirikiana na waume zao wakati wa uhai wao.

Kwa mujibu wa takwimu za baadhi ya mashirika ya Kikosi kazi  kama Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) takribani wajane 544 wamefika katika vituo vyao mbalimbali kuomba msaada wa kisheria kwa mwaka 2011 kutokana na kudhulumiwa mali baada ya wenza wao kufariki.

Pia zipo ripoti za tafiti zilizofanywa na mashirika mbalimbali katika maeneo tofauti nchini ambazo zinaonesha wazi kwamba vitendo hivyo vimekithiri na vinaongezeka kila kukicha.

Kutokana na ripoti za ukatili ambao wanafanyiwa wajane hao katika maeneo mbalimbali nchini, hivi karibuni WLAC ilitoa tamko la kukemea vitendo hivyo kwa sababu vina madhara makubwa katika maendeleo ya taifa.

Kwa sababu inaeleweka wazi Tanzania ni miongoni nwa nchi zilizoridhia mikataba mbalimbali ya kimatifa inayohimiza ulinzi wa haki za binadamu na usawa katika jamii ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.

Kwa hiyo ni vema serikali ikaona umuhimu wa kufanya haraka kufanya marekebisho ya sheria ya mirathi kwa sababu inachangia wajane kuendelea kukandamizwa na kunyimwa stahiki zao.

Suala hili lipewe uzito kwa sababu limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu na wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na waathirika ambao wa vitendo hivyo.

Kwa sababu mfumo wa mirathi unakiuka misingi ya usawa ,umili wa mali na kuwa na maisha bora, familia na kutweza utu wa wanawake hasa wajane.

Nionavyo, jamii zetu zinapaswa kuondokana na mila potofu dhidi ya wajane na kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa ujumla kwa sababu vitendo hivyo vinakwamisha maendeleo.

Kwa sababu hata vitabu vya dini vinaeleza wazi kuwa jamii inapaswa kuwajali wajane kwa kuwapa misaada mbalimbali na siyo kuwanyanyasa na kuwapokonya stahiki zao.

Serikali pia iendelee kushirikiana na vituo hivyo kutoa elimu ya usawa na madhara ya vitendo vya kikatili ili jamii ielewe madhara yake.

Pia ingekuwa vema kama vituo vya misaada ya kisheria vingeongezwa katika maeneo yote nchini hasa vijini ambako uelewa wa masuala ya usawa ni mdogo.

Naamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee itakayowakomboa wajane kutokana na dimbwi la mateso na kuishi maisha ya furaha.

0717 157514

No comments:

Post a Comment