28 September 2012
Vurugu kubwa Arusha *Mfuasi CUF ajeruhiwa, machinga walianzisha
Na Pamela Mollel, Arusha
WAFANYABIASHARA ndogo ndogo jijini Arusha maarafu kama 'Machinga', jana wamevamia eneo la Kiwanja cha Ermoil kilichopo karibu na Soko la Kilombero baada ya kubomoa uzio wa eneo hilo na kuanza kupimiana maeno ya kufanyia biashara zao.
Tukio hilo limetokea wakati Jiji hilo likiwa na ugeni mkubwa wa watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wanashiriki mkutano wa pili wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani katika Afrika (AGRA), uliofunguliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete ukiwa na lengo la kujaribu kuleta mageuzi ya kilimo Afrika.
Hali hiyo ilisababisha vurugu ambapo mfuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Athuman Abrahaman, alijeruhiwa usoni baada ya kupigwa mawe na kundi la watu wasiofahamika.
Katika vurugu hizo, gari la matangazo la CUF nalo lilipopolewa mawe na kusababisha spika zake kuharibika vibaya ambapo majira ya saa tatu asubuhi, askari wa jiji hilo walionekana wakipita katika mitaa mbalimbali na kuwatangazia wamachinga wote kuondoka maeneo ambayo hayajatengwa kufanyia biashara zao.
Askari hao walidai kama wafanyabiashara watakaidi agizo hilo, watachukua bidhaa zao kwa nguvu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Wamachinga hao walikataa kutekeleza agizo hilo ndipo askari wa jiji walianza kusomba bidhaa hizo na kuzipakia ndani ya gari wakizipeleka katika ofisi za Manispaa ya Arusha ambapo hali hiyo iliwafanya wafanyabiashara kujikusanya pamoja na kuvamia eneo la wazi Ermoil kwa kuvunja uzio wa mabati uliokuwepo na kuanza kujigawia maeneo wakiyapima kwa kamba.
Baadhi ya wafanyabiashara walisema eneo walilokuwa awali NMC haliwafai kwa shughuli zao kwani halina miundombinu na usalama mdogo wa mali zao.
“Hapa hatuondoki hadi kieleweke, tumechoka kunyanyaswa na kunyimwa haki zetu, sisi tuna familia zinatutegemea,” walisema.
Baadhi ya wafanyabiashara walitumia fursa hiyo kupora mali mbalimbali zilizopo ndani ya eneo hilo kama mabati, nondo na saruji ambazo ni mali ya mtu anayedaiwa kumiliki eneo hilo.
Mbali ya kupora mali, walikata miti iliyokuwa ndani ya eneo hilo na kuichoma moto hivyo kusababisha moshi mzito ambapo polisi waliokuwa wakipita, waliwaangalia bila kuchukua hatua.
Inadaiwa kuwa, kitendo cha Jeshi la Polisi kushindwa kuwadhibiti wafanyabiashara hao kimechangiwa na uhaba wa askari kutokana na ugeni unaohudhuria mkutano huo pamoja na kuhofia vurugu zaidi zinazoweza kutokea.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Bw. John Mongella, alilaani tukio hilo na kudai wafanyabiashara hao wamevamia eneo ambalo si la kwao na kukitupia lawama chama kimoja cha siasa nchini akidai ndio kimehusika kuhamasisha vurugu hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa hiyo, Bw. Omary Mkombole, alisema uvamizi wa eneo hilo ni uvunjifu wa sheria na kudai wafanyabiashara hao wataondolewa hivi karibuni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
CUF tafuteni mahali ambapo kuna ngome za CCM mkaendeshe mikutano yenu.Arusha mnatafuta nini?
ReplyDelete