10 September 2012

Viongozi waadilifu chachu ya maendeleo


Na Michael Sarungi

UBAGUZI wa rangi ni moja ya vukatili unaoweza kusababisha machafuko kutokana na pande mbili kutoutiana huku kila mmoja akijiona mkubwa zaidi.

Dunia nzima ya wanapinga ubaguzi wa haki, dhuluma na unyanyasaji bado unawakumbuka watu kama akina Dk Leon Howard Sullivan, Dk Martin Luther King Jn na wengine wengi waliojitolea kupoteza uhai wao kwa kupigania maisha ya wengine na kupinga vitendo hivyo.

Dkt. Leon Sullivan alikuwa mwanaharakati aliyezaliwa Oktoba 16 mwaka 1922,  Chareston Magharibi mwa Virginia nchini Marekani na kufariki Aprili 24 mwaka 2001 Scottsdale Arizona Marekani.

Alikuwa na sifa ya kuandika vitabu vingi wakati wa uhai wake alitumia muda mwingi kuhakikisha ustawi wa jamii kubwa maskini iliyokuwa inamzunguka kwa wakati huo na alitumia Kanisa kuwaunganisha Wamarekani wenzake weusi wenye asili ya Afrika.

Wakati dunia haijasahau machungu ya kumpoteza gwiji huyo Dunia inashuhudia kumalizika kwa Mkutano wa tisa wa Jumuiya ya Leon Sulliva umemalizika katika jiji la Malabo huko Equatorial Guinea huku kukiwa na utekelezaji hasi kuhusu suala zima la kimaendeleo, kiuchumi na kidemokrasia katika bara zima la kiafrika.

Mkutano huu ni mwendelezo wa Mkutano uliomalizika nchini Tanzania katika jiji la Arusha ambao nao uliacha maswali mengi kwa wananchi wanaozifahamu kazi alizozifanya Sulivan wakati wa uhai wake.

Ni maendeleo hasi kwa kiwango kikubwa kwani hata viongozi waliokabidhiwa jukumu la kuwaongoza wenzao hawajui nini cha kufanya kuwaokoa wenzao wanaoishi chini ya mstari wa umaskini.

Leo imepita miaka 40 tangia kuuwawa kwa Martin Luther na miaka 11 tangia dunia ilipompoteza mwanaharakati mwingine mtetezi wa wanyonge Dkt. Sullivan hakika kumbukumbu za watu wengi bado zinawakumbuka wachungaji hawa.

Je katika Tanzania ya leo wanaojiita wanaharakati, viongozi wa kidini na viongozi wa serikali wana nini cha kujivunia ambacho vizazi vijavyo vitaweza kuwakumbuka na kuwaenzi kama ilivyo kwa watu kama akina Sullivan? jibu ni rahisi tu kuwa hakuna wengi wao wapo kwa maslahi yao binafsi na familia zao.

Je katika ni kiongozi gani duniani ambaye ana uhakika siku Mungu atakapomwita atakuwa na kitu cha maana cha kwenda kujivunia zaidi ya lawama za kuwaonea watu wake, kuwaibia na kuwafisadi.

Japo malengo ya wanaharakati wa miaka ya nyuma ilieleweka kuwa ni kuhakikisha ustawi wa wananchi na kuhakikisha kuwa suala zima la ustawi wa wananchi unawiana hiyo ni tofauti na miaka ya leo.

Leo tuna shuhudia watu wengi wakianzisha makanisa, vikundi vya wanaharakati kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe kimaslahi na marafiki zao, familia zao na wengine wanao wazunguka.

Kwa mara nyingi tumeshuhudia viongozi hao wakiingia katika migogoro ya kimaslahi na si kwa lengo la kuwaunganisha wananchi ambao ni waumini kama walivyofanya akina Dkt. Sullivana na wenzake wa enzi hizo.

Hakuna tena viongozi wanaotetea maslahi ya wengi iwe kwa viongozi wa dini ama viongozi wa kiserikali lililopo sasa hivi ni kila mmoja kuangalia maslahi yake binafsi na kuwaacha watu wakiishi kwenye umaskini wa kutupwa.

Viongozi wetu kuanzia wale wa kiserikali na wengine wanaonekana kutafunwa na laana ya raslimali zilizopo katika bara hili laana ambayo ni mbaya kuliko hapa duniani.

Huku hakuna utaratibu maalumu uliowekwa ya jinsi ya kugawanya na  kutumia raslimali hizo na ndiyo maana tunashuhudia machafuko mengi katika nchi nyingi za kiafrika.

Hebu angalia machafuko yanayoendelea katika nchi kama Nigeria, Afrika ya Kusini na sehemu nyingine nyingi katika bara hili kila sehemu ni vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kugombea raslimali.

Hakika hii ni laana ambayo ni lazima tukiri kuwa viongozi wetu wameshindwa kuiondoa kwani kila siku iendayo kwa mungu hali inazidi kuwa mbaya.

Kuzidi kuongezeka kwa tofauti ya kipato kati ya aliyenacho na asiye kuwa nacho ni hatari kubwa inayozidi kulinyemelea Taifa, katika hili tujiulize waliko wanazuoni wetu walio na weredi katika masuala ya kiuchumi.

Haki ni mbaya na wala haihitaji kuwa mtaalamu wa masuala ya kiuchumi kuelewa kuwa watanzania wana kabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi kwani kila sekta ni vilio vya ugumu wa maisha anzia kwa waalimu, madaktari na idara nyingine hakuna penye unafuu.

Ni heri miaka ile ya kwanza ya uhuru ingawa hatukuwa na wasomi wengi wa kada mbalimbali lakini angalau viongozi wa miaka hiyo walikuwa ni wale waliokuwa na utu wa kuwajali wengine kuliko hawa tulionao leo.

Ndiyo maana imefikia wakati wananchi wengi wanahoji umuhimu wa kuwa na watu wanaojiita wasomi wanaotumia usomi wao kuwaumiza wengine kwani watuhumiwa wote wa ufisadi ni wale wanao jiita wasomi.

Hii kwa kiwango kikubwa imesababisha kila mtanzania amekuwa ni mtu wa kulalamika kuanzia kwenye kata, mitaa, ofisini na sehemu zote za kazi kila mahali ni kulalamika.

Lakini cha ajabu ni kuwa hakuna hata mmoja aliye tayari kuondoa malalamiko hayo hata kama hadha hiyo inamhusu yeye mwenyewe udhaifu huu umeenda mpaka kwa viongozi wetu nao ni kulalamika.

Hebu fikiria kama mkuu wa mkoa naye anapopaza sauti kuwa Mkoani kwake kuna njaa, vijana hawataki kufanya kazi, majambazi wanaongezeka je kwa mwananchi wa kawaida kilio chake akipeleke wapi?

Waziri mwenye dhamana ya uvuvi anapolalamika kuwa Uvuvi haramu umeongezeka, mwingine masuala ya utalii anapo lalamika kuwa majangili wanaendeleza uwindaji haramu je kuna matumaini sehemu kama hapo? jibu ni hakuna.

Na mwisho nimalize makala hii kuwaasa  hasa Watanzania  kuacha unafiki wa kutumia mamilioni ya fedha za walala hoi  kuwakumbuka na kuwaenzi watu kama akina Dk Sullivan, Mwalimu nyerere na wengine wengi walio kuwa viongozi wa kweli.

Ufike wakati kwa viongozi wetu kuanzia wale wa kidini na kiserikali kujifunza na kuufanyia kazi uzalendo walio kuwa nao watu kama  mchungaji Martin L. King na Dkt Sullivan ambao dunia bado inawakumbukwa kwa wema wao na si kwa maovu walio acha hapa duiani.



No comments:

Post a Comment