11 September 2012

Wadau wakerwa na 'watalii' wa Olimpiki


Na Amina Athumani

WADAU wa riadha nchini wameshangazwa na wanariadha walioshiriki Olimpiki, kutoshiriki mashindano ya Taifa yaliyomalizika juzi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wanariadha wakongwe alisema wao kama wadau wa riadha hawakutegemea kuona wanariadha hao wanashindwa kushiriki mashindano Taifa kwa kuwa wao ni wanariadha wa Tanzania ambao pia wanastahili kupimwa uwezo wao.

"Tulitegemea wote tungewona hapa uwanjani na wao wakiangaliwa uwezo wao, lakini cha kushangaza hawakutokea na sijaona mwanariadha yeyote mkongwe aliyekimbia zaidi ya hawa chipukizi," alisema mdau huyo.

Hata hivyo alipoulizwa Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui juu ya kutokuwepo kwa wanariadha hao, alidai ni vyema wakaulizwa wenyewe sababu zilizowafanya wasishiriki mashindano hayo.

Pia Nyambui alisema wanariadha walioshiriki Olimpiki walikimbia mbio ndefu za kilometa 42 (Marathon), ambapo katika mashindano hayo hazikuwepo.

Naye mmoja wa viongozi wa RT, ambaye pia hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema baadhi ya wanariadha hao walikwenda kushiriki mbio za Safari Marathon zilizofanyika Arusha, ambazo zilikuwa na zawadi ya fedha taslimu hali iliyosababisha wakongwe kuyakwepa na kukimbilia kwenye michuano hiyo.

Alisema kitendo hicho kimeukera uongozi wa riadha na huenda wakayafungia mashindano ya Safari Marathon kwa mwakani kuwa hawakupaswa kuandaa mashindano hayo siku moja na ya taifa.

Mashindano ya Taifa yalimlizika juzi huku Mjini Magharibi ya Zanzibar, wakiendelea kushikilia taji hilo kwa miaka miwili mfululizo.

No comments:

Post a Comment