10 September 2012

Mradi wa urutubishaji udongo utaongeza uzalishaji mazao




Na Kassian Nyandindi

WAHENGA husema kilimo ni uti wa mgongo na kinaongoza kwa kuajiri watu wengi na kuliingizia taifa fedha za kigeni.


Ni kupitia mazao mbalimbali ya biashara kama vile kahawa, pamba, korosho na mengine yamekuwa yakiuzwa ndani na nje ya nchi hivyo kuchangia katika jitihada za kukuza pato na uchumi wa nchi.

Pia mazao ya chakula yamekuwa yakizalishwa na wakulima katika maeneo mbalimbali, na kuwafanya watu waondokane na adha ya baa la njaa.

Kutokana na kutambua umuhimu wa kilimo cha mazao ya chakula na biashara, serikali imekuwa ikijitahidi kuweka mazingira mazuri ili wakulima wake waweze kutekeleza majukumu yao bila ya matatizo.

Njia mojawapo ambayo imekuwa ikifanywa na serikali ni kuhakikisha inaandaa wataalamu wa kutosha katika sekta hiyo muhimu, ambao wamekuwa wakipelekwa kwenye vijiji na kata ili hatimaye waweze kutoa elimu kwa wakulima, ikiwa ni lengo la kuzalisha mazao bora ambayo mwisho wa siku hupata bei nzuri sokoni.

Miradi mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza kilimo imekuwa ikipata wafadhili kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa na kuondokana na kilimo cha  zamani au cha mazoea ambacho kimsingi hakimletei tija mkulima.

Kupitia miradi hiyo wakulima wamekuwa wakipata fursa ya kujifunza mambo ya kimsingi ambapo mwisho wa siku hujikuta wakinufaika jambo ambalo limekuwa ni faraja, na sio kwao tu bali hata kwa taifa hili kwa ujumla.

Mradi wa urutubishaji husishi wa udongo unaotekelezwa katika wilaya tatu za mkoa wa Ruvuma, kwa ushirikiano wa taasisi ya utafiti wa kilimo Uyole chini ya wizara ya kilimo chakula na ushirika halmashauri hizo ni za Mbinga, Namtumbo na Songea vijijini kwa kushirikisha wakulima.

Kijiji cha Mahande kilichopo katika kata ya Utiri wilayani Mbinga mkoani hapa, ni miongoni mwa vijiji nane vinavyoshirikiana na watafiti kutoka taasisi ya utafiti wa kilimo Uyole (Mbeya) katika urutubishaji wa udongo kwa kutumia mazao jamii ya mikunde ili hatimaye wakulima waweze kuongeza uzalishaji wa mazao.

Mazao yanayoelekezwa kwa wakulima ni mahindi na soya ambapo lengo kuu ni kuboresha lishe na kuongeza kipato katika ngazi ya kaya.

Kikundi cha Mapatano chenye wanachama kumi, huku wanawake wakiwa sita na wanaume wanne kilianza mwaka 2010 ambapo kwa muda wote huo kimekuwa kikishirikiana na watafiti hao.

Pamoja na mambo mengine wakulima kutoka sehemu mbalimbali huenda katika kikundi na kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa wakulima wenzao ambao wamepata mafanikio baada ya kuwemo ndani ya kikundi hicho.

“Kazi ya utafiti ilianza mwaka 2010 kila mkulima katika kikundi chetu alikuwa analima jumla ya ploti 5 za ukubwa wa mita za mraba 100 ambapo ploti tatu zilikuwa zinalimwa mahindi kwa kutumia aina tatu za mbolea”, anasema Bi. Balbina Nchimbi Katibu wa kikundi hicho.

Anasema mbolea za kupandia ambazo zinatumika kupandia ni za Minjingu chenga, Minjingu mazao na DAP na kwamba mbolea za kukuzia zilizokuwa zinatumika ni S/A na UREA kwa viwango vilivyokuwa vinapendekezwa na wataalamu wa ugani.

Anasema kuwa baada ya kupanua uelewa wa matokeo ya matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa mahindi na soya kwa msimu wa mwaka 2011 na 2012 kila mkulima amelima nusu ekari ya mahindi na nusu ekari ya zao la soya.

Naye Bi. Katarina Nkwera ambaye ni mmoja kati ya wanachama anasema wakulima wamejifunza matumizi sahihi ya mbolea, mbegu bora, nafasi sahihi za upandaji na kupalilia kwa wakati mwafaka jambo ambalo huchangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la mahindi.

Anasema pamoja na mafaniko waliyopata kutokana na utafiti huo bado kuna changamoto ambazo wakulima zinawakabili ikiwemo kutopatikana kwa soko la uhakika wa zao la mahindi na soya.

Changamoto nyingine ni riba kubwa za mikopo kutoka katika taasisi za kifedha na uelewa mdogo wa jamii, kubwa ni la wakulima juu ya matumizi sahihi ya soya katika lishe.

Kaimu meneja wa mradi wa urutubishaji husishi wa udongo kutoka chuo cha kilimo Uyole Bw. William Mmari anasema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mkoani Ruvuma mwaka 2009 na kwamba umefadhiliwa na shirika la mapinduzi ya kijani Africa(AGRA).

Bw. Mmari anasema kuwa mradi huo unalenga kuwafikia wakulima 30,000 ndani ya miaka mitatu ambapo mpaka sasa umewafikia zaidi ya wakulima wadogowadogo 10,000.

Anafafanua kuwa baada ya wakulima kujifunza na kuona umuhimu wa matumizi ya mbolea za kupandia, kukuzia na mzunguko wa mazao ya mahindi, soya na karanga jinsi mbinu hizi zinavyoongeza uzalishaji mradi uliwaunganisha wakulima hawa na taasisi za kifedha.

Anasema kuwa taasisi hizo huwakopesha wakulima fedha ili kununua pembejeo za kilimo, ikiwemo mbegu bora na mbolea ambapo baadaye hurejesha mikopo pamoja na riba.

Kwa mujibu wa Bw. Mmari mradi pia umewafundisha wakulima mafunzo ya kilimo biashara, matumizi ya mikopo ili waweze kulima na kuuza kwa faida, na kurejesha mikopo na kwamba wajenge tabia ya kujiwekea akiba hali itakayowafanya kilimo chao kuwa endelevu.

Anataja mafunzo yaliyotolewa kwa wakulima hao kuwa ni urutubishaji husishi na faida zake, kilimo bora cha mahindi, soya na karanga, usindikaji wa soya, kutengeneza unga wa lishe, keki, maandazi, maziwa, mikate lengo ikiwa ni kuboresha lishe na kipato kwenye kaya.

Kuhusu wakulima wanaokopa anasema mradi unamwekea mkulima akiba kidogo kwenye akaunti yake ili benki au SACCOS iweze kumkopesha na kwamba mkulima huyo analazimika kuwafundisha wakulima wengine wasiopungua 30.

Anasema kuwa mpaka sasa wakulima 370 wamenufaika na mpango huo wa kukopa na kurejesha kwa wilaya zote tatu za Namtumbo, Songea vijijini na Mbinga huku lengo likiwa ni kuwafikia wakulima walio wengi zaidi.

Mradi huo umekuwa ukitafuta taasisi za kifedha sambamba na wasambazaji wa pembejeo za kilimo, ambao husambaza kwa wakulima hao ambapo mkataba huwa baina ya taasisi ya utafiti Uyole, mkulima na msambazaji wa pembejeo hizo.

Bw. Mmari ambaye pia ni mtafiti wa kilimo kutoka Uyole anabainisha kuwa AGRA pia wameshatoa ufadhili kwa miradi miwili ya afya ya udongo ambapo mmoja unatekelezwa katika mkoa wa Ruvuma na mwingine mkoani Mbeya.

Anasema wakulima 10,000wamenufaika na mradi wa urutubishaji husishi wa udongo ambapo njia mojawapo iliyotumika ni ya mafunzo ya darasani kwa wakulima viongozi na mashamba darasa.

Anataja njia zingine kuwa ni kupitia maonesho ya wakulima ambayo kiwilaya na kila kijiji kwa kila mwaka hufanyika, kutembeleana baina ya wakulima na kwamba wakulima viongozi kwa kushirikiana na wagani wameweza kufundisha wakulima wengi.

Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa na wakulima kupitia mradi wa urutubishaji husishi wa udongo kwa wakulima wa wilaya hizo tatu za mkoa wa Ruvuma, bado wana changamoto kubwa ya kuhakikisha wale ambao wamepata mafunzo wanawaelimisha wakulima wengine kupitia vikundi au mashamba darasa.



No comments:

Post a Comment