07 October 2011

Walemavu watishia kuandamana kudai makontena

Na Anneth Kagenda

CHAMA Cha Walemavu kwa kushirikiana na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na Kutoa Huduma Bure kwa Walemavu (UDF), kimeandaa maandamano ya
Amani kwenda Wizara ya Fedha kuishinikiza serikali kuwajibika kulipia gharama ya sh. milioni 120 ya ushuru ya makontena matatu yaliyoko bandarini.

Akizungumza katika Ofisi za gazeti hili Dar es Salaam jana,Mratibu wa UDF Taifa, Bw. Enock Bigaye, alisema maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika Oktoba 16 mwaka huu kuanzia Mnazi Mmoja hadi Wizara ya Fedha saa 4:00 asubuhi.

Alisema maandamano hayo ya Amani yatafanyika ili kuangalia uwezekano wa kupata makontena hayo ambayo hadi sasa yamefikisha siku 362 na kila siku ushuru wa makontena hayo unaongezeka kutokana na kuendelea kukaa huko.

"Kila siku kontena moja linagharimu dola 40 na hii ni kutokana na tulipunguziwa, kwa vifaa hivyo ni vya watu wenye ulemavu mbalimbali lakini kila yanavyozidi kukaa ndivyo gharama yake inavyoongezeka," alisema Bw. Bigaye.

Alisema makontena hayo yaliyotoka nje ya nchi kama msaada kwa walemavu  yakiwa yamesheheni vitu mbalimbali zikiwamo baiskeli za walemavu, fimbo, miwani, poda, mafuta maalum ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kofia na vingine vingi.

"Kupitia kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili wa Viongozi wa Umma chini ya sheria namba 13 ya 1995 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 5 ya 2001,inayompa kibali kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa sheria ya maadili ya viongozi wa umma tunaomba Kamishina wa Hazina awajibike kwa kutolipa ushuru wa makontena yetu kwa muda stahiki hivyo kufikia muda wote huo," alisema Bw. Bigaye.

Alidai Mratibu huyo alifika kwenye vyombo vya habari kulalamikia ucheleweshwaji wa makontena hayo na kuiomba Serikali kuingilia kati kwa madai kwamba vifaa hivyo vinatakiwa kuwafikia wahusika lakini hadi muda huo bado vilikuwa vinashikiliwa na Mamlaka ya Bandari nchini.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu kuhusu madai hayo Msemaji wa Wizara ya Fedha Bi. Ingiaedi Mduma, alisema kimsingi kundi hilo halina sababu ya kuulalamikia Wizara hiyo na kwamba wanapaswa kuzungumza na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

"Serikali inafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo, hao wanapaswa kuzungumza na TPA na si Wizara ya Fedha, nakumbuka hilo suala walishaelekezwa,"alisema.

No comments:

Post a Comment