24 September 2012

Viongozi UWT wapongezwa kwa sherehe



Na Goodluck Hongo

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, jana kimefanya sherehe kubwa ya kuwapongeza wajumbe wapya wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), akiwemo Mwenyekiti wake, Bi. Florence Masunga.


Sherere hizo zilianza saa saba mchana katika ukumbi wa Urafiki ambapo mamia ya wanawake wa chama hicho kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam walihudhuria.

Akiwashukuru wanachama wa jumuiya hiyo, Bi. Masunga, alisema uchaguzi umekwisha hivyo kilichobaki ni wana CCM kuunganisha umoja wao ili kutekeleza sera za chama.

Alisema zipo changamoto nyingi ambazo ziko mbele yake sambamba na kuhakikisha anawakomboa waanawake kiuchumi na kuiwezesha CCM kuibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Didas Masaburi na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Yusufu Mwenda.

Sherehe hizo zimefanyiwa wakati aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti, Bi. Anna Hangaya, akiwa amekata rufaa kwa Katibu Mkuu wa CCM, kupinga matokeo yaliyompa ushindi Bi. Masunga na kutaka yatenguliwe akidai uchaguzi huo ulitawaliwa na rushwa.

Katika madai hayo, Bi. Hangaya alisema siku ya uchaguzi Septemba 9 mwaka huu, wagombea waligawa fedha hadharani kwa wajumbe.

Baadhi ya wajumbe walidai kuwa, kufanyika kwa sherehe hizo wakati chaguzi nyingine zikiendelea ngazi ya Wilaya na mikoa hakuimarishi umoja wa wana CCM kama inavyodaiwa.

No comments:

Post a Comment