24 September 2012

Mtanzania aipa ubingwa Roiet United ya Thailand


Na Zahoro Mlanzi

MTANZANIA Michael Victor 'Vieira', ameisaidia timu yake ya Roiet United kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Pili nchini Thailand mara mbili mfululizo baada ya kupachika mabao 20 katika mechi 32.

Mchezaji huyo anayecheza soka la kulipwa nchini humo, alisajiliwa na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro na pia alikuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana (U-20) baada ya kulelewa na kilichokuwa Kituo cha Michezo Tanzania (TSA).

Akizungumza kwa simu na gazeti hili kutoka Thailand jana, Vieira alisema anajisikia fahari kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo kwani hakutarajia kama angeweza kucheza soka katika timu hiyo kutokana na ushindani uliokuwepo.

"Asikudanganye mtu maisha popote na namshukuru mungu nimevumilia sana na kama si kufanya mazoezi kwa bidii nisingefika hapa nilipo, hivi ni chaguo la kwanza la kocha wangu na kila anaponipa nafasi huwa simuangushi," alisema Vieira.

Alisema wametwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 60 huku timu za Sisaket United ikifuata ikiwa na pointi 59, Udon Thai FC ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 56, Loei City ina pointi 54 na  Nakhonphanom FC ina pointi 51.

Alisema kwa upande wa wafungaji bora wa kwanza anatoka katika timu yao ambapo amefunga mabao 28, wa pili ana mabao 26, wa tatu ana mabao 23 na yeye (Vieira) ana mabao 20.

Alisema baada ya kutwaa ubingwa huo, sasa timu yao itacheza Ligi Daraja la Kwanza la nchi hiyo huku hivi sasa inakabiliwa na mashindano ya 'Championi' ambayo hushindanisha bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa pili na bingwa wa ligi yao na mshindi wa pili kwa mechi za nyumbani na ugenini.

Akizungumzia kuhusu kurudi nchini kwa mapumziko, Vieira alisema hatoweza kurudi kwa sasa mpaka michuano hiyo itakapomalizika ambapo inatarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu.

Timu hiyo ilianzishwa mwaka 2008 na inatumia uwanja wa Roi Et wenye uwezo wa kuchukuwa watazamaji waliokaa kwenye viti 2,500.

No comments:

Post a Comment