28 September 2012
Utata maiti iliyozikwa kimakosa wamalizwa
Na Stella Aron
SAKATA la mwili wa marehemu Ntimaruki Khenzidyo (25), uliochukuliwa katika mazingira ya kutatanisha kwenye Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam na kwenda kuzikwa Handeni, mkoani Tanga kwa taratibu za Kiislamu, limepatiwa ufumbuzi baada ya mwili huo kurejeshwa kwa wanafamilia na hatimaye kuzikwa Makaburi ya Mikocheni Chama.
Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu jana walifurika katika Hospitali ya Mwananyamala kushuhudia maiti hiyo ambayo jana imezikwa kwa taratibu zote za Kikristo.
Mwili huo ulidaiwa kuchukuliwa kimakosa na kwenda kuzikwa Kijiji cha Msima ambapo juzi ulifukuliwa baada ya ndugu zake kukamilisha taratibu za kisheria na kurudishwa Dar es Salaam.
Taratibu za kutoa heshima za mwisho zilifanyika katika hospitali hiyo ambapo ibada ya mazishi iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Wasabato, Mwanyamala, Joshua Magoiga.
Baada ya kuaga mwili huo, safari ya kwenda makaburini ilianza ambapo waombolezaji walikua wakiimba nyimbo za kumshukuru Mungu kutokana na mwili wa ndugu yao kurejeshwa.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya ndugu wa marehemu walionekana kutoridhishwa na utaratibu unaotumiwa na hospitali hiyo ambao ndio chanzo cha mwili huo kuzikwa kimakosa mkoani Tanga.
Bw. Efraim George, alisema kama uongozi wa hospitali hiyo utaendelea na utaratibu mbuvu wa kutoa maiti hospitalini hapo, makosa mengi kama hayo yataendelea kutokea.
Kaka wa marehemu Bw. Fredrick Muyoba, alisema ni vyema Serikali ikaubadilisha uongozi wa hospitali hiyo kwani si mara ya kwanza maiti kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Sofinus Ngonyani, alisema awali taratibu za kuchukua maiti hiyo zilifuatwa wakiwemo ndugu wa marehemu, askari na madaktari walioufanyia uchunguzi.
Alisema siku ya tukio walipokea maiti mbili za ajali zilizotokea Tegeta na Kawe, jijini Dar es Salaam ambapo marehemu wote majina yao hayakuweza kufahamika ambapo hali hiyo ndio ilisababisha mkanganyiko wa uchukuaji wa maiti.
Maiti hiyo ilifukuliwa kutokana na kibali kilichotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na ufukuaji huo ulisimamiwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni na mhudumu wa Hospitali ya Mwananyamala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment