28 September 2012

Dk. Mkopi: Sijaitisha mgomo wa madaktari



Na Rehema Mohamed

RAIS wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dkt. Namala Mkopi, amekana kuitisha mgomo wa madaktari kupitia chama hicho.

Dkt. Mkopi ambaye anakabiliwa na kesi ya kudharau Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, alikana madai hayo wakati akisomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na wakili wa Serikali Bw. Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Faisal Kahamba wa Mahakama hiyo.

Upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa, kesi hiyo ililetwa ili upande wa jamhuri uweze kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kinyume na kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na kosa la pili
kuwashawishi madaktari kufanya mgomo.

Ilidaiwa kuwa, Juni mwaka huu madaktari wanaofanyakazi katika hospitali za Serikali, walifanya mgomo dhidi ya mwajiri wao ambao uliandaliwa na MAT.

Madaktari hao waligoma kuhudumia wagonjwa wakati mkataba wao wa ajira ambao waliongia na Serikali ni kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa.


Bw. Kweka alidai kuwa, wakati mgomo huo ukiendelea, Serikali ilipeleka maombi namba 73 ya mwaka 2012 katika Mahakama Kuu Diveshini ya Kazi ili itoe amri ya kuzuia mgomo huo usiendelee hadi mgogoro kati yao na MAT ambao ulifunguliwa kwenye Tume ya Usuluhishi wa Migogoro (CMA), utakapomalizika.

Alidai Juni 22 mwaka huu, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ilitoa amri ya kuwataka madaktari waliogoma nchi nzima wasitishe mgomo ambapo nakala ya amri hiyo alipewa mshitakiwa (Dkt. Mkopi), Juni 25 mwaka huu.

Aliongeza kuwa, licha ya mshitakiwa kupatiwa nakala ya amri hiyo ambayo aliipokea pamoja na madaktari wenzake, bado waliendeleza mgomo huo.

Juni 26 mwaka huu, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ilitoa amri nyingine kwa MAT iliyokuwa ikiwataka watekeleze kwa vitendo amri ya Mahakama iliyotolewa Juni 22 mwaka huu ikimtaka Dkt. Mkopi kwenda kwenye vyombo vya habari na kuwatangazia madaktari wote waliogoma wasitishe mgomo huo.

Alisema Dkt. Mkopi alishindwa kutekeleza amri hizo matokeo yake yeye na madaktari wenzake wakaendelea na mgomo ambapo Julai 9 mwaka huu, mshitakiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo Julai 10 mwaka huu na kufunguliwa kesi.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Dkt.Mkopi, alikanusha kuwa yeye si daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ila alikubali kuwa ni daktari wa binadamu.


Dkt. Mkopi pia alikanusha madai ya madaktari kugoma kuwatibia wagonjwa na si kweli kwamba alidharau amri ya mahakama ya Juni 22 mwaka huu iliyomtaka aende kwenye vyombo vya habari kuwatangazia madaktari waache mgomo.

Hakimu Kahamba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23 mwaka huu, ambapo siku hiyo kesi itakuja kwa ajili ya mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.

No comments:

Post a Comment