28 September 2012
Usiku wa sauti na Diamond Sound sasa mwezi ujao
Na Amina Athuman
ONESHO la usiku wa sauti na marafiki wa kweli litakalowakutanisha wanamuziki mbalimbali waliowahi kupiga bendi ya Diamond Sound ‘Dar es Salaam Kibinda Nkoi’ pamoja na wanamuziki wengine nyota nchini litafanyika mwezi ujao.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Endless Fame inayoandaa onesho hilo, Zulfa Msuya alisema Dar es Salaam jana kuwa, kusogezwa mbele kwa onesho hilo kumetokana na baadhi ya wanamuziki kuwa safarini huku wengine wakiwa katika kazi za kurekodi na bendi zao.
“Tumelazimika kusogeza mbele onesho hili kwa sababu walengwa wakuu walikuwa safarini, wengine walikuwa wana kazi ya kurekodi, kwa hiyo hawakuweza kuanza mazoezi kwa muda uliotakiwa, lakini sasa wamesharejea wote na wako tayari kuanza kambi kwa ajili ya siku hiyo,” alisema.
Zulfa alisema wanamuziki hao watakuwa wakifanya mazoezi katika ukumbi wa Princess Hall pale Sinza, Mapambano na mazoezi hayo yatachukuwa wiki mbili.
Naye kiongozi wa Diamond Sound, Ibonga Katumbi ‘Jesus’ alisema wanataka kufanya onesho ambalo litakuwa la historia, hivyo bila timu yote kukamilika isingekuwa rahisi wao kuanza mazoezi.
“Sisi hatujakaa pamoja zaidi ya miaka 12, ili kupata muziki wenye kiwango cha juu ni lazima tukae si chini ya wiki mbili kufanya mazoezi, ili watu wasikie ladha ile ile waliyokuwa wakisikia TCC, Silent Inn.
“Wasisahau kuwa tutapiga pia nyimbo za Beta Musica, sasa mtu kama Adolph hakuwepo Beta, Kata Nyama amepiga Beta wimbo mmoja, lakini kuna wanamuziki kaka zetu watakuwepo pia nyimbo zao ni za miaka ya 1980 huko nao lazima zifanyiwe mazoezi, tuko makini kuhakikisha tunafanya hili kwa ufanisi mkubwa,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment