18 September 2012

Usalama wa wanafunzi Shule ya Msingi Kahama hatarini


Na Patrick Mabula, Kahama

MAJENGO ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Kahama, mkoani Shinyanga, yapo katika hali mbaya kiusalama kutokana na uchakavu wa kuta na paa zake.


Hali hiyo inahatarisha maisha ya wanafunzi 1,934, kwani tangu ujenzi wa shule hiyo ukamilike mwaka 1953, baadhi ya vyumba vyake havijawahi kufanyiwa ukarabati hadi sasa.

Taarifa iliyotolewa na mwalimu wa shule hiyo, Bi. Esther Nyamhanga kwa niaba ya Mkuu wa shule, kutokana na hali hiyo wanafunzi hujikuta wakisoma katika mazingira magumu.

Bi. Nyamhanga aliyasema hayo mbele ya Mbunge wa jimbo hilo, Bw. James Lembeli wakati akikabidhi msaada wa madawati 70 yaliyotokana na michango ya wafadhili, madiwani na wazazi.

Alisema mbali ya vyumba vya madarasa, jengo la utawala pamoja na maktaba nayo yapo katika hali mbaya ambapo wakati wa masika paa zake huvujisha maji na kuingia ndani kutokana na uchakavu wake.

“Matatizo mengine yanayoikabili shule hii ni upungufu wa matundu ya choo 53, yaliyopo ni 18, madawati 644 na vyumba vya madarasa mahitaji 48 ambapo vilivyopo 18.

“Shule hii ilijengwa na wananchi wenye asili ya India na iliitwa Indian School ambapo wanafunzi walikuwa wa asili ya hiyo ila baada ya kupata uhuru ikachukua wanafunzi mchanganyiko,” alisema Bi. Nyamhanga.

Kwa upande wake, Bw. Lembeli, aliwataka viongozi na wananchi kuacha itikadi ya kisiasa katika mambo ya maendeleo badala yake wachangie elimu ambayo ndiyo msingi wa maisha.

Katika hafla hiyo, Bw. Lembeli alifanya harambee kwa wazazi na viongozi ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji huo aliahidi kuboresha shule hiyo, kujenga madarasa matano na kutoa fedha taslimu sh. milioni 1.4.

Bw. Lembeli alitoa sh. milioni 1.5, kada wa CCM, Bw. Shida Sokko sh. 500,000, waandishi wa habari 60,000 ambapo jumla ya pesa zote  zilizopatikani zilikuwa sh. milioni 5.2.

No comments:

Post a Comment