18 September 2012

Askofu: Jitokezeni kutoa maoni Katiba Mpya


Na Jovither Kaijage, Ukerewe

WAKAZI wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, wamehimizwa kujitokeza na kutoa maoni yao kwenye tume inayoratibu mchakato wa kupata Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa ya Watanzania.


Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrea Gulle, alitoa wito huo juzi mjini Nansio wilayani hapa katika ibada maaalumu.

Katika ibada hiyo, Askofu Gulle alifanya maombi maalumu ya kumuingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Ukerewe, Mchungaji Elias Lugaganya na kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya mtumishi wa usharika huo.

Alisema waumini wa kanisa hilo wanapaswa kutambua kuwa, katiba ndio muongozo wa maisha yao hivyo aliwasihi waone umuhimu wa kujitokeza na kutoa maoni yao ili kupata katiba yenye tija.

Katika hatua nyingine, Askofu Gulle aliwataka waumini wa kanisa
hilo kuepuka matendo machafu hasa ya ndoa za jinsia moja na mambo yasiyozingati maelekezo ya Mungu.

“KKKT linapinga ndoa za jinsia moja hivyo waumini mnapaswa kuwa makini na baadhi ya makanisa yanayoanzishwa sasa yenye matendo yanayokwenda kinyume na maandiko matakatifu.

“Hivi karibuni yameanzishwa makanisa yanayofanya ibada kwa matendo yasiyofaa ambapo viongozi wao hubebwa mgongoni na waumini mengine yakihalalisha viongozi wao kuzini na waumini,” alisema Askofu Gulle.

Aliongeza kuwa, mbali ya mafundisho hayo kuwa kinyume na kitabu cha Biblea, pia yanakiuka haki za binadamu na yanaweza kueneza magonjwa kama UKIMWI.

Kwa upande wake, Mchungaji Lugaganya aliwataka viongozi wa kanisa hilo kuendelea kuelimisha waumini wao juu ya madhara ya matendo hayo ili kuwa na jamii yenye maadili na afya njema.

No comments:

Post a Comment